Msemaji wa Serikali Charles Owino amewakashifu viongozi wa upinzani kwa kuingilia sera za serikali tawala, akiwataka badala yake kuwasilisha mipango na suluhisho kwa Wakenya.
Akizungumza wakati wa Kikao na wanahabari mnamo Agosti 26, 2026, katika kikao chake cha kwanza rasmi tangu ateuliwe kuchukua nafasi ya Dkt. Isaac Mwaura, Owino amepuuzilia mbali wito wa baadhi ya viongozi wa upinzani wa kutupilia mbali Mamlaka ya Afya ya Jamii, SHA.
Owino amesema SHA si mpango wa Rais William Ruto bali ni mamlaka iliyoanzishwa chini ya Sheria ya Bima ya Afya ya Jamii na haiwezi kuondolewa kiholela akiwataka wapinzani kuelezea Wakenya namna watakavyoboresha huduma za afya badala ya kuahidi kuutupilia mbali mfumo huo.
“Nataka kuwaambia, yeyote atakayekuwa Rais, hata kama si Rais Ruto, hawezi kuiondoa SHA,” amesema Owino.
Aidha amesema zaidi ya Wakenya milioni 31 tayari wamejisajili katika mfumo huo, huku akikiri kuwa SHA imekumbwa na changamoto za utekelezaji.
Owino amesema serikali iko tayari kufanya marekebisho yanayohitajika, ila maamuzi hayo yanapaswa kuongozwa na ukweli wala si siasa.
Wakati uo huo, amelaani matumizi ya lugha ya matusi na mashambulizi binafsi dhidi ya Rais William Ruto, hasa kwenye mitandao ya kijamii.
“Inasikitisha sana, kuwasikia baadhi ya vijana nchini wakimtukana Mkuu wa Nchi. Una maadili gani? Ni mfano gani unaowaonyesha vijana wengine katika jamii?” amehoji Owino.
Hata hivyo, Owino amesema Wakenya wana haki ya kuwa na mitazamo tofauti ya kisiasa, akiwataka kufanya hivyo kwa heshima na kudumisha heshima ya taasisi za serikali.









