Ruto Atenga Sh1.2 Bilioni Kujenga Chuo Kikuu Emurua Dikirr KItakachopewa jina la Marehemu Johanna Ngeno.

0

Rais William Ruto ametangaza mipango ya kutenga shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya ujenzi wa chuo kikuu kipya kwenye eneobunge la Emurua Dikirr kaunti ya Narok, kitakachopewa jina la aliyekuwa Mbunge wa eneo hilo, marehemu Johana Ngeno.

Akizungumza katika soko la kisasa la Mamboleo, Ruto amesema fedha hizo zitatumika kujenga chuo hicho baada ya wakazi wa eneo hilo kuomba serikali kuanzisha chuo kikuu.

“Leo nimewaletea shilingi bilioni 1.2 za kujenga chuo kikuu hapa Emurua Dikirr, ambacho kitaitwa kwa jina la ndugu yetu Johana Ngeno. Chuo kikuu hicho nitakachojenga kitawasaidia watoto kutoka hapa Emurua Dikirr na maeneo mengine ya Kenya,” amesema.

Ruto pia ametangaza shilingi milioni 180 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ya wanafunzi, akisema miradi hiyo itapanua fursa za elimu, kuunda nafasi za ajira na kuchochea uwekezaji katika eneo hilo.

“Leo pia ninazindua ujenzi wa mabweni kwa ajili ya vijana wetu. Tumetenga shilingi milioni 180 kwa ajili ya kutekeleza kazi hiyo,” ameongeza.

Rais William Ruto pia ametangaza mipango ya kuboresha barabara inayowahudumia wakazi wa eneobunge hilo, pia, imetenga fedha za ujenzi wa barabara mpya ya kiwango cha kimataifa, itakayoanzia Salgaa kupitia Chebole, Abosi na Shartuka hadi Emurua Dikirr.

Aidha amesema ujenzi wa barabara hiyo utaanza baadaye mwaka huu, huku uzinduzi rasmi wa mradi huo ukipangwa kufanyika mwezi Oktoba.

“Nitakuja kuzindua ujenzi huo mwezi Oktoba,” amesema Ruto.

Ziara ya Rais William Ruto katika eneobunge la Emurua Dikirr inajiri siku chache baada ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kutembelea eneo hilo.

Ziara ya Gachagua ilikuwa sehemu ya kampeni za kuhamasisha chama chake cha DCP, huku akilenga kupanua ushawishi wake wa kisiasa kuelekea uchaguzi wa 2027.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here