Kenya roho juu kutetea ubingwa wa bara

0

Timu ya taifa ya Voliboli (Malkia Strikers) imevuna ushindi wa pili mfululizo katika Mashindano ya Afrika ya Voliboli ya Wanawake ya CAVB baada ya kuifunga Mali seti tatu kwa nunge Alhamisi jioni tarehe 27 Agosti 2026 jijini Nairobi.

Kenya iliwalaza mabinti wa Mali 25-17, 25-10, 25-18 katika uwanja wa nyumbani wa Kasarani Indoor Arena, huku seti ya kwanza ikiwa yenye ushindani mkubwa zaidi katika mchezo huo.

Mali ililingana na Malkia Strikers kwa pointi 15-15 kabla ya Kenya kujitenga na kuchukua seti hiyo kwa 25-17.

Seti ya pili ilionekana kuwa rahisi zaidi kwa Kenya, ambayo iliizuia Mali kufikisha zaidi ya pointi 10, hata hivyo, Mali iliongeza upinzani katika seti ya tatu, lakini Kenya iliendelea kuongoza na kushinda 25-18 na kukamilisha ushindi wa seti zote tatu.

Matokeo hayo yanafuatia ushindi wa Kenya wa 3-0 dhidi ya Zambia katika mchezo wao wa kwanza wa kundi A Jumanne, huku Mali ikipoteza mfululizo baada ya kulazwa 3-1 na Zambia.

Matokeo hayo mawili yamewaweka malkia hao wanaonolewa na mkufunzi Geoffrey Omondi kileleni mwa Kundi A, ambalo sasa lina timu tatu baada ya Morocco kujiondoa kwenye mashindano.

Kenya iliingia kwenye mashindano hayo ikiwa mabingwa watetezi baada ya kuifunga Misri 3-0 katika fainali ya mwaka 2023 mjini Yaoundé Cameroon.

Ubingwa wa mwaka huu una umuhimu zaidi, kwani mabingwa wa Afrika watapata tiketi ya kushiriki michezo ya Olimpiki ya Los Angeles 2028, huku timu tatu bora zikifuzu kwa Kombe la Dunia la Volleyball (FIVB) la mwaka 2027.

Misri pia iliendeleza mwanzo wake mzuri Alhamisi kwa kuifunga Uganda 3-0, huku Rwanda ikiifunga Burundi kwa matokeo kama hayo.

Senegal nayo ilipata ushindi wake wa kwanza katika mashindano hayo baada ya kuifunga Burkina Faso kwa seti 25-17, 25-14, 25-20, huku Algeria ikikamilisha ushindi mwingine wa seti tatu bila kupoteza kwa siku hiyo baada ya kuifunga Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) 3-0.

Timu 15 zinashiriki mashindano hayo katika makundi manne, kundi B likikutanisha Misri, Uganda, Burkina Faso na Senegal.

Cameroon, ambayo imeshinda ubingwa mara tatu, inaongoza Kundi C pamoja na Nigeria, Tunisia na Ghana, huku kundi D likiwa na Rwanda, Algeria, DRC na Burundi.

Mashindano hayo yanafanyika Nairobi kuanzia Agosti 25 hadi Septemba 5, huku Kenya ikiwa mwenyeji wa michuano ya Afrika kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 11.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here