Wanaofadhili Vurugu Za Kisiasa Wachukuliwe Hatua Rais Aamuru.

0

Rais William Ruto amekashifu vikali vurugu za kisiasa zinazoshuhudiwa nchini, akisema vitendo vya vurugu vinavyofadhiliwa kisiasa havina nafasi katika demokrasia ya Kenya.

Akizungumza katika hafla ya kuhitimu kwa maafisa wa Huduma ya Polisi katika Chuo cha Mafunzo ya Polisi cha Kiganjo, Kaunti ya Nyeri, mnamo tarehe 28 Agosti 2026, Rais Ruto amezitaka asasi zote za usalama kuchukua hatua thabiti dhidi ya wanaofadhili, kupanga au kuchochea vurugu za kisiasa.

“Msikamawate vijana wanaobeba silaha pekee na kumwacha mtu aliyewaajiri, kuwasafirisha na kuwalipa bila kuwajibishwa. Hakuna mwanasiasa anayestahili kuwa na kikosi chake binafsi, wala hakuna mgombea mwenye haki ya kuwatisha wananchi.”

“Vurugu za kisiasa hazina nafasi katika demokrasia yetu. Huduma ya Kitaifa ya Polisi pamoja na asasi zingine za usalama zinapaswa kuchukua hatua thabiti, halali na bila upendeleo dhidi ya yeyote anayefadhili, kupanga, kuchochea au kutekeleza vurugu za kisiasa.” Amesema Rais.

Rais amesisitiza kuwa ushindani wa kisiasa unapaswa kuzingatia sera huku wananchi wakiwa huru kuchagua viongozi wanaowataka.

“Ushindani wa kisiasa ni muhimu kwa demokrasia yetu. Vyama vina uhuru wa kujipanga, wagombea lazima wawe huru kufanya kampeni, na wananchi wawe huru kufanya uchaguzi wao.” Ameongeza Rais.

Aidha Rais amewaagiza maafisa wa usalama kuimarisha ulinzi kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027, akisema Polisi wana jukumu la kikatiba la kulinda nafasi ya kidemokrasia ya wananchi.

“Polisi wana jukumu la kikatiba la kulinda nafasi ya kidemokrasia ya wananchi.” Rais ameeleza.

“Wakati uo huo, sheria lazima itekelezwe kwa weledi na kwa kuheshimu maisha na utu wa kila mwananchi.

“Nchi salama ni ile ambayo mama anaweza kutembea kuelekea nyumbani bila hofu, mfanyabiashara akaendesha biashara yake bila vitisho, familia ikalala kwa amani, na mwananchi akaweza kutoa maoni yake, kuhudhuria mikutano ya kisiasa na kupiga kura bila kulazimishwa.”

“Hivyo ndivyo Katiba inavyotekelezwa katika maisha ya kila siku, pale ambapo haki zilizoainishwa katika sheria kuu ya nchi zinapodhihirika katika maisha ya kila mwananchi.” Amebainisha Rais.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here