Kindiki Ataka Suluhu ya Haraka kwa Mgomo wa Wauguzi.

0

Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki ametoa wito kwa Wizara ya Afya, Baraza la Magavana na Tume ya Kuhakiki Mishahara ya Wafanyikazi wa Umma (SRC), kushauriana na muungano wa wauguzi ili kupata suluhu ya kudumu ya mgomo unaoendelea.

Akizungumza wakati wa kikao maalum cha Baraza la Bajeti na Uchumi la Serikali za Kitaifa na Kaunti (IBEC) mtaani Karen, jijini Nairobi, hii leo Agosti 31 2026, Kindiki ameonya kuwa mgomo wa kitaifa wa wauguzi unaoendelea unaweza kuvuruga zaidi utoaji wa huduma za afya kote nchini.

“Ninatoa wito kwa Wizara ya Afya, Baraza la Magavana na Tume ya Mishahara ya wafanyikazi wa umma (SRC) kushirikiana na miungano ya wauguzi na kukamilisha mchakato huo, kwa sababu hatutaki kuvurugwa kwa huduma za afya.” Ameeleza Kindiki.

Wauguzi wanataka kukamilishwa kwa mazungumzo kuhusu mkataba wa pamoja CBA ya mwaka 2025-2029 pamoja na utekelezaji wa miongozo mipya ya maendeleo ya taaluma yao miongoni mwa maswala mengine

Naibu wa Rais pia ameitaka Tume ya SRC kufanya uhakiki wa kina wa mishahara na marupurupu katika sekta ya umma.

Aidha ameeleza kuwa tofauti kubwa za mishahara kati ya wafanyakazi wa vyeo vya juu na wale wa vyeo vya chini zinaweza kuchochea migogoro ya kikazi miongoni mwa wafanyakazi katika serikali ya kitaifa na za kaunti

“Tunapaswa pia kuzingatia mchakato unaoendelea wa mapitio ya mishahara. Ni lazima tuwe waangalifu ili tusijenge tofauti kubwa za mishahara kati ya maafisa wa vyeo vya juu na wale wa vyeo vya chini.” Amesema Kindiki.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here