Rais William Ruto amemteua rasmi Dkt. Duncan Ojwang Oburu kuwa mwenyekiti mpya wa Mamlaka Huru ya Uangalizi wa Polisi (IPOA).
Kwa mujibu wa notisi maalum iliyochapishwa kwenye gazeti rasmi la serikali la tarehe 31 Agosti 2026, rais Ruto amemteua Ojwang kuongoza mamlaka hiyo kwa kipindi cha miaka sita.
Uteuzi huo unamweka Ojwang katika uongozi wa IPOA, mamlaka iliyoanzishwa kisheria kwa jukumu la kutoa usimamizi wa kiraia wa utendaji wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS).
Rais William Ruto alimteua Dkt. Ojwang kujaza nafasi hiyo mnamo Julai, 2026 na kuwasilisha jina lake kwa bunge ili kuzingatiwa.
Bunge la Kitaifa liliidhinisha uteuzi wake licha ya utata ulioibuliwa kuhusu iwapo alikuwa amehitimu, pamoja na madai ya kwamba alikosa baadhi ya vyeti vilivyohitajika kisheria.
Wakati wa kikao cha kusailiwa mnamo Agosti 12, 2026, Dkt. Ojwang aliahidi kulinda uhuru wa IPOA, akisema atauheshimu na kuudumisha atakapokuwa akitekeleza majukumu ya mamlaka hiyo.
“Ninaamini mimi ni jasiri. Nasema ukweli. Nikabidhini jukumu hilo. Tutasema ukweli kwa mamlaka,” Dkt. Ojwang aliambia kamati ya idara ya utawala na usalama wa ndani ya bunge la kitaifa.
Aliambia kamati hiyo, inayoongozwa na mbunge wa Narok Magharibi, Gabriel Tongoyo, kwamba kuna haja ya uwiano kati ya uhuru wa kiutendaji wa IPOA na ushirikiano na Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS).
Alisema baadhi ya majukumu ya IPOA, yakiwemo uchunguzi, yanahitaji uhuru kamili, huku majukumu mengine kama ukaguzi, mageuzi na ushirikiano na maafisa wa polisi yakihitaji ushirikiano.
“Linapokuja suala la utovu wa nidhamu, utovu wa nidhamu unaoripotiwa, kukagua operesheni na kufanya uchunguzi, uamuzi na uhuru wa IPOA katika utendaji na kufanya maamuzi hauwezi kuiruhusu kupokea maagizo kutoka kwa inspekta jenerali,” alisema.
Dkt. Ojwang sasa anamrithi jaji Ahmed Issack Hassan, aliyeacha wazi nafasi hiyo mnamo Februari 17, 2026 baada ya kuteuliwa kuwa jaji wa Mahakama ya Rufaa nchini.
Naibu mwenyekiti wa IPOA, Anne Wanjiku Mwangi, amekuwa akishikilia nafasi hiyo kama kaimu.









