Timu ya taifa ya wanawake ya voliboli (Malkia Strikers) imefuzu awamu ya nusu fainali ya mashindano ya ubingwa wa bara Afrika baada ya kutoka nyuma na kulaza Algeria kwa seti 3-1 katika mechi ya robo fainali iliyochezwa katika ukumbi wa uwanja wa kimataifa wa michezo wa Kasarani jijini Nairobi Jumanne usiku tarehe 1 Septemba 2026.
Algeria ilianza vyema kwa kushinda seti ya kwanza kwa alama 25-21, hali iliyowalazimu Malkia Strikers wanaonolewa na kocha Geoffrey Omondi kurejea mchezoni na kusawazisha.
Malkia walijibu kwa nguvu katika seti ya pili, wakishinda kwa alama 25-7, kabla ya kuongeza ushindi mwingine wa 25-15 katika seti ya tatu.
Mabingwa hao tetezi walikamilisha ushindi wao katika seti ya nne kwa alama 25-18, licha ya juhudi kubwa za Algeria kurejea mchezoni.
Ushindi huo umewakutanisha Kenya ambao ni wenyeji na mabingwa wa zamani Cameroon katika mechi ya nusu fainali itakayochezwa Alhamisi terehe 3 Septemba 2026 ikiwa ni marudiano ya mwaka 2023 yaliyofanyika jijini Yaoundé ambapo Kenya iliwanyamazisha mbele ya mashabiki wa nyumbani kabla ya kutwaa ubingwa wake wa kumi.
Cameroon ilitinga hatua hiyo baada ya kuibuka na ushindi mfululizo wa seti 3-0 dhidi ya Uganda, kwa alama 25-18, 25-20 na 25-18.
Awali, Misri, mabingwa mara tatu na washindi wa fedha katika mashindano ya mwaka 2023, iliendeleza kiwango chake kizuri baada ya kuifunga Tunisia kwa seti 3-0 na kutinga nusu fainali, ambapo itakutana na Rwanda.
Rwanda nayo ilifuzu kwa hatua ya nne bora baada ya kuichapa Ghana kwa seti 3-1, kwa alama 25-17, 24-26, 25-19 na 25-18.









