‘Dogo’, mkenya wa pili kucheza ligi ya mabingwa – Ulaya

0

Nahodha wa timu ya taifa ya soka (Harambee Starlets), Mwanahalima “Dogo” Adam, ameandikisha historia, baada ya kuwa mchezaji wa pili mkenya kufuzu kwa hatua ya Ligi ya Klabu Bingwa Barani Ulaya – UEFA kwa wanawake (UWCL).

Mshambuliaji huyo amefikia hatua hiyo ya kihistoria baada ya klabu yake ya Denmark, HB Køge Women, kupata ushindi wa jumla wa mabao 2-1 dhidi ya vigogo wa Uholanzi, PSV Eindhoven, katika mechi ya mchujo iliyokuwa na ushindani mkubwa Jumatano tarehe 2 Septemba 2026.

HB Køge iliweka msingi wa kufuzu kwa ushindi wa bao moja kwa bila katika mchezo wa kwanza uliochezwa nchini Uholanzi, ambapo ilionyesha kiwango bora cha uchezaji na kujinyakulia faida muhimu.

Katika mchezo wa marudiano nchini Denmark, Mwanahalima na wachezaji wenzake walistahimili presha kubwa na kupata sare ya bao moja kwa moja, na hivyo kushinda kwa jumla ya mabao 2-1 na kufuzu kwa mashindano ya klabu za ngazi ya juu barani Ulaya.

Uelewa wake wa mbinu za mchezo pamoja na juhudi zake kubwa katika safu ya ushambuliaji vilikuwa muhimu katika mechi yote mbili, akisaidia HB Køge kuvuka moja ya vikwazo vigumu zaidi katika hatua ya mchujo na kujiunga na timu 16 bora za Ulaya.

Mafanikio hayo yanaongeza sura nyingine muhimu katika historia ya soka la wanawake nchini Kenya kwenye jukwaa la kimataifa.

Mwanahalima anafuata nyayo za mshambuliaji nyota Marjolen Nekesa, ambaye mwaka 2023 alikuwa mwanamke wa kwanza kutoka Kenya kucheza katika hatua kuu ya UWCL akiwa na klabu ya vigogo wa Jamhuri ya Czech, Slavia Prague.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here