Uhaba wa maziwa ni wa muda; serikali yasema

0

Wizara ya Kilimo imehusisha upungufu wa sasa wa maziwa katika soko na hali mbaya ya hewa inayochangiwa na ukame unaotangulia mvua zinazotarajiwa za El Niño.

Katibu Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Mifugo, Jonathan Mueke, amesema Alhamisi tarehe 3 Septemba 2026 kuwa ukame unaoendelea nchini umeathiri malisho ya mifugo na hivyo kusababisha kupungua kwa uzalishaji wa maziwa.

‘‘Kabla tuu ya mvua za El Niño, kwa kawaida huwa tunashuhudia kipindi cha ukame. Haijaathiri Kenya pekee yake bali maeneo mengine duniani. Hii imeathiri malisho yetu na hivyo kusababisha hali iliyopo.’’ Mueke alisema.

Mueke aliongeza kuwa serikali imekubaliana na wadau wote katika mnyororo wa thamani wa sekta ya maziwa kuwaunga mkono wakulima ili kukabiliana na changamoto hiyo.

Aliongeza kwamba kwa kuwa tatizo kubwa kwa sasa ni uhaba wa chakula cha mifugo kutokana na ukosefu wa mvua, serikali itafanya mazungumzo na watengenezaji wa chakula cha mifugo kutafuta suluhu.

Amesema serikali pia imekubali kuruhusu uagizaji wa mahindi ya kutengeneza chakula cha mifugo bila kutozwa ushuru, huku akiongeza kuwa agizo hilo linatarajiwa kuchapishwa rasmi katika gazeti la serikali wiki ijayo.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa Chama cha Wasindikaji Maziwa, Kenneth Gitonga, amesema wametathmini takwimu zilizopo na kubaini kuwa hali hiyo ni ya muda tu.

Gitonga amesema suluhu ni kuwaunga mkono wakulima, huku wasindikaji wakiahidi kuhakikisha kila tone la maziwa linalozalishwa linakusanywa na kufikia soko.

Amesema hakuna haja ya wananchi kuwa na hofu, akiwataka washirikiane kutumia kiwango cha maziwa kilichopo kwa sasa.

Hali hii inajiri wakati ambapo wakazi wa Nairobi na maeneo mengine nchini wameripoti kukabiliwa na upungufu wa maziwa, wafanyabiashara wakisema usambazaji umepungua, huku baadhi ya maduka yakiripoti ongezeko la bei.

Katika taarifa, Bodi ya Maziwa nchini imefafanua kuwa kiwango rasmi cha maziwa yaliyowasilishwa kwa wasindikaji kilipungua kwa asilimia 3.7, kutoka lita milioni 84.4 mwezi Juni hadi lita milioni 81.3 mwezi Julai 2026.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here