Timu ya taifa ya Voliboli (Malkia Strikers) imesalia hatua moja zaidi kutwaa kwa mara ya 11, ubingwa wa Mashindano ya taifa bingwa barani Afrika kwa Wanawake 2026 baada ya kuwalaza wapinzani wao Cameroon kwa seti tatu mfululizo katika ukumbi wa ndani wa uwanja wa kimataifa wa michezo wa Kasarani Alhamisi tarehe 3 Septemba jioni, na hivyo kutinga fainali.
Uchezaji bora wa kikosi cha mkufunzi Geoffrey Omondi uliwawezesha kuzima juhudi za Cameroon za kurejea mchezoni na kupata ushindi wa mnono wa seti 25-19, 25-20, 25-20.
Mshambuliaji Terry Tata, wa Malkia Strikers alionesha kiwango cha hali ya juu ya mchezo, akiwa mfungaji bora wa siku kwa kupata pointi 14.
Ushindi huo ulikuwa sawa na ule wa nusu fainali ya mwaka 2023 jijini Yaoundé, ambapo Kenya iliifunga Indomitable Lionesses ya Cameroon kwa seti 3-1 na kutwaa taji lao la kihistoria la 10-barani Afrika.
Ushindi dhidi ya Cameroon ulikuwa ujumbe mwingine unaodhihirisha ubabe wa Kenya katika ushindani ambao kwa miaka mingi umekuwa ukitawala Voliboli ya wanawake barani Afrika.
Kenya na Cameroon zimekuwa zikipishana kwa utwaaji wa taji la Afrika mara kwa mara, huku Malkia Strikers wakilitwaa tena mwaka 2023.
Kenya itakutana na Misri katika fainali ya Ijumaa tarehe 4 Septemba baada ya nchi hiyo ya Afrika Kaskazini kuilaza Rwanda kwa seti 3-0 katika nusu fainali ya kwanza.
Mapema Alhamisi, Misri ilihakikisha nafasi yake ya kucheza fainali baada ya kuishinda Rwanda kwa seti 3-0 (25-5, 25-17, 32-30).
Sasa macho yote yanaelekezwa Kasarani kwa pambano kuu la kutafuta medali ya dhahabu, huku Kenya ikilenga kutumia faida ya kucheza nyumbani na kutetea taji hilo kama bingwa tetezi dhidi ya Misri ambayo kwa upande mwingine inalenga kubadilisha medali yake ya fedha ya mwaka 2023 kuwa dhahabu.
Katika fainali hiyo Kenya itategemea uungwaji mkono mkubwa wa mashabiki wa nyumbani huku ikilenga kurudia ushindi wake wa seti 3-0 dhidi ya Misri mwaka 2023 na kutetea ubingwa wake.
Mashindano ya mwaka 2026 yanafanyika Nairobi, huku washindi wa mashindano hayo wakipata pia tiketi ya moja kwa moja ya kushiriki Michezo ya Olimpiki ya Los Angeles ya mwaka 2028.









