
Wakenya wametakiwa kuwa waangalifu kutokana na kuendelea kuenea kwa virusi vya MPOX nchini.
Wizara ya Afya imesema inaendelea kuimarisha ufuatiliaji na hatua za kukabiliana na maambukizi, huku wananchi wakihimizwa kuchukua tahadhari zinazohitajika kujilinda.
Akizungumza wakati wa kikao cha usimamizi wa Idara ya Afya ya Umma, Katibu wa Afya ya Umma Mary Muthoni amesema MPOX bado ni tishio kwa afya ya umma.
“Tunawahimiza wananchi kuzingatia kiwango cha juu cha usafi wakati wote.” Amesema Muthoni.
Kulingana na Muthoni, Kenya imerekodi visa 1,298 vilivyothibitishwa vya MPOX na vifo 19 katika kaunti 40.
“Kuhusu MPOX, tumerekodi visa 1,298 vilivyothibitishwa na vifo 19 hadi sasa. Kaunti 40 kati ya 47 nchini zimeathiriwa na ugonjwa huo.” Ameongeza.
Kufikia sasa, kaunti saba, zipo katika hatari kubwa ya kupata virusi hivyo ambavyo hadi sasa vimesababisha vifo vya watu 19 nchini.
Kaunti ya Mombasa inaongoza katika kaunti zilizoathiriwa kwa visa 452 ikifuatiwa na Kaunti ya Nairobi yenye visa 320 na kufuatiwa na Kaunti ya Busia ikiwa na visa 115.
Nyingine ni; kaunti za Makueni, Kiambu, Kilifi na Nakuru.
“Tunazo kaunti zinazoongoza kwa idadi ya visa, ambapo Mombasa inaongoza, ikifuatiwa na Nairobi, Busia, Makueni, Kiambu, Kilifi na Nakuru.”
Aidha Amesisitiza haja ya uhamasishaji endelevu pamoja na uchunguzi ulioboreshwa katika sehemu zote za mpaka wa nchi.
Ingawa Kenya haina virusi vya Ebola vilivyothibitishwa, Muthoni amesema kuna hatua zilizowekwa ili, kuhakikisha kwamba virusi hivyo haviingii nchini.








