Msomi maarufu wa sheria nchini Profesa PLO Lumumba ameeleza wasiwasi kuhusu migogoro inayoshuhudiwa katika maeneo mbalimbali barani Afrika.
Lumumba amesema kwa sasa kuna karibu migogoro 40 barani humu, akisema hali hii inaonyesha changamoto zinazolikabili bara la Afrika katika kushughulikia migogoro yake.
“Hivi sasa kuna karibu migogoro 40 barani Afrika. Hiyo ndiyo hali ya Afrika. Angalia tunakosuluhisha migogoro yetu. Tunakwenda Doha na Istanbul kusuluhisha migogoro yetu.” Amesema Lumumba.
Aidha ametaja Mataifa ya Ethiopia, Sudan, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Somalia na Cameroon kuwa miongoni mwa nchi zinazokabiliwa na migogoro.
Lumumba amesema bara la Afrika halijaishi kulingana na kile kilichokusudiwa wakati Umoja wa Afrika, AU, ulipoanzishwa mwaka 1963.
Amesema Afrika inapaswa kujipanga kupitia Umoja wa Afrika, AU, ili iweze kuwa na sauti moja na kusikika katika masuala ya kimataifa.
“Ikiwa Afrika inataka kusikika, inapaswa kujipanga kupitia Umoja wa Afrika. Hawajajipanga kiasi kwamba hakuna anayewasikiliza.” Ameongeza.
Lumumba pia amehoji wito wa baadhi ya viongozi wanaotaka Afrika kupewa viti viwili vya kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, akiuliza ni nchi zipi zitakazowakilisha bara hilo.
Amesema Afrika bado haizungumzi kwa sauti moja, akisisitiza umuhimu wa bara hili kujipanga zaidi kupitia Umoja wa Afrika ili liweze kuwa na msimamo unaosikika katika masuala ya kimataifa.









