Serikali Yashinikizwa Kufichua Aliko Mwaipaya.

0
Mwanaharakati wa Tanzania Twaha Mwaipaya

Vuguvugu la Linda Mwananchi limeshinikiza kuachiliwa kwa mwanaharakati wa upinzani kutoka Tanzania Twaha Mwaipaya na kufanyika kwa uchunguzi huru kuhusu madai ya kutekwa nyara kwake katika eneo la Kamulu, kaunti ya Machakos.

Hatua hiyo inajiri huku kukiwa na hofu kwamba huenda akarejeshwa Tanzania kwa lazima.

Mwaipaya anadaiwa kutekwa nyara mnamo Jumapili tarehe 25 mwezi Oktoba 2026 alipokuwa akisafiri kwa teksi kwenda kuwatembelea marafiki.

Shirika la kutetea haki za kibinadam la Amnesty International Kenya na Muungano wa Watetezi wa Haki za Kibinadamu (Defenders Coalition) zimesema watu waliohusika walikuwa wakitumia magari matatu, yakiwemo gari aina ya Toyota Land Cruiser Hardtop.

Mashirika hayo yamewaomba wananchi wenye taarifa zinazoweza kusaidia kumpata Mwaipaya kujitokeza na kuzifikisha kwa mamlaka husika, huku shinikizo likiongezeka kwa serikali ya Kenya kubaini kilichotokea na kuhakikisha usalama wake.

“Ni lazima mamlaka zibaini aliko haraka na kuhakikisha usalama wake,” imesema shirika la Amnesty International Kenya.

Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu, Oktoba 26, 2026, Linda Mwananchi imelalamikia tukio hilo, ikilihusisha na visa vya awali vya kutekwa kwa viongozi wa upinzani na watetezi wa haki za kibinadamu kutoka mataifa jirani wakiwa nchini Kenya.

Vuguvugu hilo limerejelea kisa cha kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Dkt. Kizza Besigye aliyetekwa nyara jijini Nairobi mnamo Novemba 2024 na kupelekwa Uganda, ambako alifikishwa mbele ya mahakama ya kijeshi.

Besigye bado anazuiliwa, huku kukiwa na wasiwasi kuhusu afya yake na mazingira anamoishi akiwa kizuizini.

Pia limetaja tukio la kutekwa kwa mwanaharakati wa Tanzania, Maria Sarungi Tsehai, na watu waliokuwa na silaha jijini Nairobi mnamo Januari 2025.

Sarungi aliachiliwa saa chache baadaye kufuatia ghadhabu ya umma na uingiliaji kati wa watetezi wa haki za kibinadamu.

Sarungi, ambaye amekuwa akiikosoa serikali ya Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, ameeleza wasiwasi kwamba Mwaipaya anaweza kuwa hatarini iwapo atarejeshwa Tanzania.

Sarungi anadai kuwa Mwaipaya alikimbilia Kenya baada ya kutekwa nyara na kuteswa na polisi nchini Tanzania.

“Ikiwa Twaha atavushwa na kupelekwa Tanzania, watamuua!” amesema Sarungi.

Sarungi mwenyewe anadaiwa kutekwa katika eneo la Kilimani, jijini Nairobi, Januari 12, 2025, kabla ya kuachiliwa baadaye siku hiyo akieleza kuwa serikali ya Tanzania ilihusika na kutekwa kwake.

Tukio la hivi punde limeibua tena wasiwasi kuhusu usalama wa wakosoaji wa serikali na watetezi wa haki za kibinadamu kutoka mataifa jirani wanaokimbilia Kenya kutafuta hifadhi.

Vuguvugu hilo pia limekosoa kile lilichokitaja kuwa kuendelea kwa serikali kudhoofisha uhuru wa kidemokrasia, likionya kuwa namna wakosoaji wanavyotendewa nchini Kenya inaweza pia kuhatarisha watu wanaotafuta ulinzi nchini humu.

“Tunalaani mwenendo usio wa kidemokrasia wa utawala wa Rais Ruto.” Imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Linda Mwananchi imetaka uchunguzi huru kuhusu kutekwa kwa Mwaipaya na hatua za uwajibikaji kuchukuliwa dhidi ya wote waliohusika, bila kujali nyadhifa zao au uraia wao.

“Tunahitaji kufichuliwa mara moja aliko Mwaipaya, uchunguzi huru kuhusu kutekwa kwake na uwajibikaji kwa wote waliohusika, bila kujali nyadhifa zao au uraia wao,” imeongeza taarifa hiyo.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here