Kenya yafuzu raundi ya mchujo kombe la dunia

0

Timu ya taifa ya kandanda kwa wasichana wasiozidi umri wa miaka 17, (Junior Starlets) imeandikisha historia ingine kwa kufuzu kwa mara ya kwanza katika hatua ya 16 bora ya Kombe la Dunia la FIFA baada ya kuishinda Samoa mabao 4-0 katika mechi yao ya mwisho ya Kundi E nchini Morocco.

Katika mechi iliyochezwa Jumapili tarehe 25 Oktoba 2026, Mwanakombo Bakari alifunga mabao mawili, huku Brenda Awuor na Gaudancia Maloba wakifunga bao moja kila mmoja, na kuiwezesha Kenya kupata ushindi wake wa kwanza katika mashindano hayo kwenye uwanja wa Mohammed VI Football Academy.

Ushindi huo mkubwa, ukiambatana na matokeo ya mechi kutoka makundi mengine, uliihakikishia Kenya nafasi ya mwisho iliyokuwa ikipatikana katika hatua ya 16 bora, ikiwa mojawapo ya timu nne zilizomaliza katika nafasi ya tatu zenye matokeo bora zaidi.

Ushindi huo uliogeuza hali iliyokuwa ikionekana kama kuondolewa mapema kwenye mashindano na kuwa mafanikio ya kihistoria kwa taifa baada ya Kenya kupoteza mechi mbili ya hatua ya makundi.

Mafanikio hayo yanaashiria mara ya kwanza kwa timu ya Kenya kuvuka hatua ya makundi katika Kombe la Dunia na pia kuongeza hatua ingine muhimu katika rekodi inayozidi kukua ya kocha mkuu Mildred Cheche, ambaye alikua kocha wa kwanza kuiongoza timu ya kandanda ya Kenya kushiriki Kombe la Dunia la FIFA mwaka wa 2024 akiwa na timu hiyo hiyo.

Kenya iliingia katika mechi hiyo ikiwa chini ya shinikizo baada ya kuanza kampeni yake kwa kupoteza mabao 3-0 dhidi ya China, kabla ya kukubali kichapo cha mabao 6-1 dhidi ya Marekani.

Vipigo hivyo viwili vilididimiza imani ya Kenya kusonga mbele kwa kuhitaji ushindi wa kuridhisha dhidi ya Samoa, pamoja na matokeo mazuri kutoka kwa mechi nyingine, ili kuendeleza matumaini yake ya kufuzu kwa hatua ya mchujo.

Hata hivyo, mfumo wa kufuzu kwa timu zilizomaliza katika nafasi ya tatu zenye matokeo bora zaidi uliacha nafasi ndogo ya matumaini, na Junior Starlets wakaitumia kwa kufanya vizuri dhidi ya Samoa.

Bakari aliweka msingi wa ushindi kwa kufunga bao la mapema kabla ya kuongeza bao lake la pili kipindi cha pili huku Awuor akiingia kwenye orodha ya wafungaji kabla ya mapumziko, na kuipa timu ya Cheche msingi imara ilipokuwa ikisaka ushindi mkubwa ambao ungeongeza nafasi zake za kufuzu.

Maloba aliongeza bao jingine huku Kenya ikiendelea kutawala mchezo, kabla ya Bakari kukamilisha mabao yake mawili na kuhitimisha alasiri ya kukumbukwa kwa timu hiyo.

Tofauti ya mabao manne ilikuwa muhimu katika juhudi za Kenya za kufuzu, kwani iliimarisha kwa kiasi kikubwa uwiano wake wa mabao baada ya vipigo vikubwa dhidi ya China na Marekani.

Kufuzu kwa Kenya pia kulitegemea matokeo ya mechi katika makundi mengine, huku mechi za mwisho za hatua ya makundi zikiamua timu zilizomaliza nafasi ya tatu ambazo zingefuzu.

Kufuzu kwa Kenya kulithibitishwa baadaye, huku FIFA ikitangaza kuwa Junior Starlets walikuwa wamechukua nafasi ya mwisho iliyokuwa ikipatikana katika hatua ya 16 bora.

Junior Starlets sasa watakutana na Japan, iliyomaliza kileleni mwa Kundi D, katika hatua ya 16 bora kuendeleza safari yao ya Kombe la Dunia.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here