
Rais William Ruto amesema serikali yake itaendelea kuunga mkono wawekezaji wanaoingia nchini, akisisitiza kuwa inalenga kuondoa vikwazo vinavyokwamisha uwekezaji, kubuni fursa za ajira na kukuza uchumi.
Akizungumza katika hafla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa kiwanda cha saruji chenye thamani ya shilingi bilioni 70 eneo la Ngaaie, Kaunti ya Kitui, Rais Ruto amesema serikali yake iko tayari kushirikiana na wawekezaji wote bila kuwanyima fursa za kuanzisha na kuendeleza biashara nchini.
“Ninawahakikishia kila mwekezaji kuwa anaungwa mkono na Serikali ya Kenya chini ya uongozi wangu.” Ruto amesema.
Rais pia ametaja mradi wa kusafisha mafuta unaohusishwa na mfanyabiashara Aliko Dangote katika Kaunti ya Lamu, wenye thamani ya shilingi trilioni 2.2, akisema una uwezo wa kufungua fursa zaidi za kiuchumi.
“Fursa hizo hazitokani tu na mradi wa Dangote wa Lamu, bali pia na miradi mbalimbali ya maendeleo ya miundombinu inayotekelezwa kote nchini.” ameongeza.
Kadhalika amewataka Wakenya kuangazia manufaa mapana ya uwekezaji badala ya kile alichokitaja kuwa propaganda kuhusu umiliki wa hisa katika kiwanda hicho cha saruji.
“Ninawaomba wananchi wa Kenya kuangazia manufaa mapana ya uwekezaji na namna unavyoweza kufungua fursa za kiuchumi na ajira nchini, bila kujali ni nani anayezibuni.” Amesema.
Kauli ya Rais inajiri huku viongozi wa upinzani wakiibua maswali kuhusu baadhi ya wawekezaji wanaoletwa nchini, wakitaka mikataba ya uwekezaji iwe wazi na kuhakikisha inalinda maslahi ya taifa badala ya kunufaisha watu binafsi.








