Rais William Ruto ametangaza kuwa serikali inapanga kuzindua kiwanda cha kwanza cha uzalishaji wa chuma nchini katika Kaunti ya Taita Taveta ndani ya wiki mbili hadi tatu zijazo, katika juhudi za kupunguza utegemezi wa malighafi kutoka nje ya nchi.
Akizungumza Jumanne, Oktoba 27, 2026 wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa kiwanda cha Saruji cha klinka eneo la Ngaaie, Kaunti ya Kitui, Ruto amesema mradi huo unaongozwa na mwekezaji wa humu nchini na utatumia madini ya chuma yanayopatikana nchini.
Rais amesema atahudhuria binafsi uzinduzi wa kiwanda hicho, akikitaja kuwa hatua muhimu katika kupanua sekta ya uzalishaji viwandani na kuongeza matumizi ya rasilimali za madini zinazopatikana nchini.
“Katika kipindi cha wiki mbili hadi tatu zijazo, nitakuwa Taita Taveta kuzindua kiwanda cha uzalishaji wa chuma, ambacho kitakuwa cha kwanza nchini,” amesema Ruto.
Ameongeza kuwa mradi huo utawezesha Kenya kuzalisha chuma kutokana na madini yake badala ya kutegemea uagizaji wa madini hayo kutoka mataifa mengine.
“Tusahau kuagiza madini ya chuma kutoka maeneo mengine. Kuanzia sasa, tutaanza kuzalisha chuma kutokana na rasilimali zilizopo nchini Kenya kwa mara ya kwanza,” amesema Rais.
Aidha, Ruto ameahidi kuwalinda wawekezaji dhidi ya kuingiliwa kisiasa.
Wakati uo huo Rais ameiagiza Wizara ya Madini kuhakikisha mikataba ya uchimbaji madini eneo la Magadi, Kaunti ya Kajiado, inatolewa kwa kampuni zilizo tayari kuchakata madini hayo nchini badala ya kusafirisha malighafi nje ya nchi.









