Gavana wa zamani wa kaunti ya Kiambu, Ferdinand Waititu, pamoja na washtakiwa wenzake akiwemo mkewe Susan Wangare, wameiomba mahakama kuwapunguzia adhabu baada ya kupatikana na hatia ya ufisadi unaohusisha shilingi milioni 588 alipokuwa uongozini.
Wakati wa vikao vya kujitetea mbele ya hakimu Harrison Barasa wa mahakama ya Milimani Jumanne tarehe 27 Oktoba 2026, Waititu aliiomba mahakama msamaha kwa makosa aliyopatikana nayo na kuitaka izingatie hali yake binafsi pamoja na ya mkewe wakati wa kuamua adhabu zao.
“Naomba msamaha kwa kosa lolote nililofanya. Mimi na mke wangu tumepatikana hatiani kwa mara ya kwanza, kwa hivyo wakati wa kutoa adhabu, tafadhali zingatieni hilo,” Waititu aliiambia mahakama.
Waititu pia aliomba mahakama kumpunguzia adhabu kutokana na nafasi yake kama mkurugenzi wa kampuni inayohusishwa na kesi hiyo akidai kwamba ilikuwa tayari ikifanya biashara kabla hajachukua wadhifa wa ugavana.
Aidha, aliiomba mahakama izingatie hali ya mkewe akisema kuwa ushiriki wake katika kampuni iliyohusishwa ulikuwa mdogo na kwamba hakuhusika moja kwa moja katika shughuli za kila siku za biashara yake.
Mawakili wa utetezi waliiomba mahakama kutathmini hali ya kila mshtakiwa kivyake badala ya kutoa adhabu zinazofanana kwa wote wakisema baadhi ya wanawake waliokuwa miongoni mwa washtakiwa walikuwa na ushiriki mdogo katika kampuni hizo na hawakuhusika moja kwa moja katika miamala ya kifedha inayochunguzwa katika kesi hiyo.
Mawakili waliomwakilisha Wangare waliiambia mahakama kuwa hakuwa mmoja wa watu walioidhinishwa kutia saini katika akaunti za benki za kampuni hiyo, wala hakuwa mnufaika wa miamala inayohusika.
Mahakama pia iliombwa kuzingatia muda ambao washtakiwa tayari wamekuwa kizuizini wakati wa kuamua adhabu zao.
Utetezi uliiambia mahakama kuwa Waititu amekuwa gerezani kwa zaidi ya mwaka mmoja, huku mshtakiwa wa nne akiwa ametumia karibu miaka miwili gerezani.
Mahakama ikiratibu kutoa hukumu tarehe 2 Novemba 2026, hoja zilizowasilishwa na utetezi zinatarajiwa kuisaidia kuamua adhabu inayofaa kwa kila washtakiwa, utetezi ukisisitiza kuwa mahakama inapaswa kuzingatia nafasi ya kila mmoja katika makosa hayo, hali zao za kifamilia, majukumu yao binafsi pamoja na muda ambao tayari wameutumia gerezani.









