Mwakilishi wa wadi ya Kileleshwa, Robert Alai, amepuuzilia mbali madai kuwa hafla ya kumbukumbu ya aliyekuwa Waziri Mkuu na mwanzilishi wa chama cha ODM, Raila Odinga huko Bondo haikuwa shughuli rasmi ya chama cha Chungwa.
Alai amesema wanachama wa ODM waliambiwa kuwa hafla hiyo ya Oktoba 15, 2026, haikuwa shughuli rasmi ya chama, hali iliyowafanya baadhi yao kutohudhuria.
Odinga alifariki dunia Oktoba 15, 2025, nchini India alipokuwa akipokea matibabu.
Kumbukumbu ya kwanza ya kifo chake ilifanyika katika uwanja wa Migwena, Bondo, kaunti ya Siaya, na kuwajumuisha wanafamilia, viongozi wa kisiasa na wafuasi kutoka mirengo mbalimbali.
Kabla ya hafla hiyo, mjane wa Raila, Ida Odinga, alikuwa ametoa wito kwa Wakenya kuweka kando tofauti za kisiasa, akisisitiza kuwa urithi wa mumewe haukuwa wa chama kimoja pekee bali wa Wakenya wote.
Ida alisema Raila alisimamia amani na umoja, akiwataka wananchi kumkumbuka kwa misingi hiyo badala ya kuzingatia tofauti za vyama vyao vya kisiasa.
Hata hivyo, Alai amesema ODM haiwezi kutenganishwa na Raila, akitaja historia ya hafla za kibinafsi za kiongozi huyo ambazo mara nyingi zilihudhuriwa na viongozi wa chama.
Alai pia amedai kuwa Mbunge wa Rarieda, Otiende Amollo, alikuwa ametangaza kuwa viongozi na wafuasi wa ODM hawakukaribishwa katika hafla hiyo.
Alai amesema ujumbe huo uliwafanya baadhi ya wanachama kuamini kuwa chama hakikupaswa kushiriki rasmi.
“Tuliambiwa na familia tusihudhurie, kwa hiyo tuliheshimu uamuzi huo. Kwanza tuliambiwa kuwa haikuwa shughuli ya ODM.” Alai amesema.
Mzozo huo sasa umeibua maswali kuhusu namna urithi wa kisiasa wa Raila utakavyohifadhiwa na nafasi ya ODM katika shughuli za kumuenzi kiongozi huyo, huku wito wa Ida wa umoja ukikabiliwa na tofauti za maoni miongoni mwa viongozi na wanachama wa chama.









