Rais William Ruto ametia saini Mswada wa Marekebisho ya Sheria za Ushuru wa mwaka 2026 na Mswada wa Marekebisho ya Mamlaka ya Ushuru nchini (KRA) wa mwaka 2026.
Rais Ruto ametia saini miswada hiyo katika Ikulu ya Eldoret, kaunti ya Uasin Gishu, Ijumaa, Oktoba 16, 2026, baada ya kupitishwa na Bunge la Kitaifa.
Kutiwa Saini kwa Miswada hiyo kuwa sheria inahakikisha kuendelezwa kwa kiwango cha chini cha VAT cha asilimia 8 kwa bidhaa za mafuta ya petroli na kuleta mabadiliko katika ushuru wa vifaa vya ujenzi pamoja na usimamizi wa mamlaka ya ushuru.
Mswada wa Marekebisho ya Sheria za Ushuru unaendeleza kiwango cha VAT cha asilimia 8 kwa petroli, dizeli na mafuta ya taa kwa kipindi cha awali cha siku 90, huku ukiruhusu kuongezwa kwa siku nyingine 90 kupitia tangazo la Gazeti Rasmi la Serikali litakalotolewa na Waziri wa Fedha John Mbadi.
Akitoa maelezo kwa Rais, Naibu Mkuu wa Wafanyakazi wa Ikulu, Josephat Nanok, amesema hatua hiyo inalenga kuwalinda Wakenya dhidi ya athari za misukosuko katika soko la kimataifa la mafuta inayohusishwa na mgogoro wa Mashariki ya Kati.
“Mswada huu kwanza unaendeleza matumizi ya VAT ya asilimia 8 kwa bidhaa za mafuta ya petroli, yaani petroli, dizeli na mafuta ya taa, ili kuhakikisha kuwa athari za mgogoro unaoshuhudiwa katika sehemu ya Mashariki ya Kati haziathiri uchumi wa Kenya” amesema Nanok.
Nanok ameongeza kuwa mashauriano na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Petroli (EPRA) pamoja na Wizara ya Kawi yalihakikisha kiwango hicho kilijumuishwa katika hesabu za bei za mafuta.
“Bila kiwango hicho cha asilimia 8 kujumuishwa, bei ya mafuta iliyotangazwa na EPRA ingekuwa ya juu zaidi kuliko ile iliyotangazwa,” ameongeza Nanok.
Sheria hiyo pia inabadilisha ushuru wa bidhaa za vigae vya ujenzi hadi shilingi 400 kwa kila mita ya mraba, na kuchukua nafasi ya mfumo wa awali uliotegemea uzito.
Aidha, inapunguza ushuru wa vifaa vya kauri (ceramic sanitary ware) vinavyotumika manymbani kutoka shilingi 50 hadi shilingi 30 kwa kila kilo.
Mswada wa Marekebisho ya Mamlaka ya Ushuru nchini (KRA) unarekebisha masharti yanayosimamia muundo na uanachama wa bodi ya KRA.
Mswada huo aidha inaweka nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari nchini (KPA) kujiunga na bodi ya KRA.
“Kwa hivyo, unamjumuisha Mkurugenzi Mkuu wa KPA katika bodi ili kuendeleza uhusiano huo na kuhakikisha kuwa maamuzi yanayofanywa na KRA yanaakisiwa pia katika shughuli za bandari,” amesema Nanok.
Marekebisho hayo pia yanaipa KRA angalau asilimia 2 ya makadirio ya mapato ya mwaka ambayo inatarajiwa kukusanya, kama yalivyoainishwa katika makadirio ya kifedha, na kusasisha orodha ya sheria zinazosimamiwa na mamlaka hiyo.
Mabadiliko hayo yanalenga kuwalinda watumiaji dhidi ya shinikizo la bei za mafuta, kupunguza baadhi ya gharama za ujenzi na kuimarisha uratibu kati ya ukusanyaji wa mapato na shughuli za bandari.









