Balozi wa Israel apiga kura Nairobi kushiriki uchaguzi utakaoandaliwa Oktoba 27

0
Balozi wa Israel nchini Kenya Gedion Behar alipokuwa akishiriki upigaji kura kwenye ubalozi Nairobi.

Balozi wa Israel nchini Kenya Gedion Behar ameshiriki zoezi la mapema la upigaji kura jijini Nairobi kwa wanadiplomasia wa taifa hilo katika uchaguzi wa nchi hiyo utakaofanyika tarehe 27 Oktoba 2026.

Katika mahojiano na wanahabari Behar alisema kuwa uchaguzi huo utaamua muundo wa bunge la Israel, (Knesset), lenye wajumbe 120, ambapo vyama vya kisiasa hujadiliana kuhusu kuunda muungano wa serikali na kumchagua waziri mkuu.

“Tunafurahi sana na tunajivunia kuwa hapa Nairobi kupiga kura na kushiriki katika mchakato wa kidemokrasia nchini Israel,” alisema Behar.

Wakati wa zoezi hilo lililofanyika Alhamisi tarehe 15 2026, katika ubalozi wa taifa hilo, Behar alibainisha kuwa takriban watu milioni 7.3 walitarajiwa kupiga kura nchini Israel, yenye idadi ya raia wapatao takriban milioni 10 akifafanua kuwa raia wenye umri wa miaka 18 na zaidi wanaweza kushiriki katika uchaguzi bila kujali dini au jinsia.

Behar alitaja masuala kama changamoto za kiusalama, migogoro ya kikanda na masuala ya kiuchumi kuwa miongoni mwa vipaumbele vinavyoweza kuathiri maamuzi ya wapiga kura.

“Mchakato huu ni wa kidemokrasia, na wengi watasema wanachotaka kusema. Kama unavyojua, kura yangu kama balozi ina uzito sawa na ya kila mtu mwingine. Nina uhakika kuwa wananchi wa Israel wamejiandaa vyema na wanajua hasa wanachotaka, na tutafurahia matokeo yoyote,” alisema balozi Behar.

Behar alisema kuwa wanadiplomasia wanaohudumu nje ya nchi hupiga kura kabla ya tarehe kuu ya uchaguzi, huku kura zao zikifungwa na kusafirishwa hadi Israel ili kujumuishwa katika hesabu rasmi ya kura.

Alieleza kuwa kura zilizopigwa jijini Nairobi zitasafirishwa kwa ndege hadi Israel kupitia njia za kidiplomasia na kufunguliwa pamoja na kura nyingine wakati wa mchakato wa kitaifa wa kuhesabu kura.

“Kura hizo zitatumwa kwa ndege hadi kwa Kamati Kuu ya Uchaguzi, na kufikia wakati masanduku yote ya kura nchini Israel yatakapofunguliwa, haya pia yatafunguliwa na kuongezwa katika jumla ya kura,” alisema.

Mpangilio huo unawahusu tu maafisa wanaostahili kupiga kura wakiwa nje ya nchi katika majukumu rasmi pamoja na wanafamilia wao wanaotimiza masharti huku raia wa kawaida wa Israel wanaoishi nje ya nchi wakihitajika kurejea moja kwa moja nchini ili kupiga kura zao.

Tofauti na mfumo wa urais nchini Kenya, ambapo wapiga kura humchagua rais moja kwa moja, waisraeli hupiga kura kwa orodha za vyama vya kisiasa vinavyowania viti katika bunge la Knesset lenye wawakilishi 120.

Baada ya matokeo kutangazwa, vyama vya kisiasa huendesha mazungumzo ili kuunda muungano wenye uwezo wa kuunda serikali.

Behar aliitaja Kenya kuwa mshirika muhimu wa Israel, akirejelea uhusiano wa muda mrefu na ushirikiano katika sekta za kilimo, elimu, afya, usalama na usimamizi wa maji.

“Tunaichukulia Kenya kama mshirika muhimu sana wa Israel,” alisema Behar, akiongeza kuwa uhusiano huo hauishii katika diplomasia rasmi pekee, bali pia unahusisha uhusiano kati ya wananchi wa nchi hizo mbili.

 

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here