Utaondoka na Ushuru wako wa Nyumba za Bei Nafuu Rais Aonywa.

0
Seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna

Seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna, amemjibu Rais William Ruto kuhusu ushuru wa nyumba za bei nafuu, akimkosoa kwa kile alichokitaja kuwa mzigo mkubwa wa ushuru unaowakabili Wakenya.

Katika chapisho kwenye mitandao ya kijamii Jumatano, Oktoba 14, 2026, Sifuna ameahidi kufutilia mbali ushuru huo punde tu upinzani utakapoingia madarakani baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2027.

“Mwaka ujao 2027, tutapunguza makato yasiyo ya lazima ya serikali ili kupunguza mzigo wa kifedha kwa wafanyakazi wote nchini Kenya. Ushuru wa nyumba utaondoka pamoja na Ruto.” Amesema Sifuna.

Aidha ameeleza kuwa kuna makato mengine yanayopaswa kujadiliwa, yakiwemo yale yanayohusiana na mfumo wa afya wa SHA.

“Amemaliza kulalamika kuhusu shilingi elfu 24 ninazolipa kwa ushuru wake wa nyumba? Kwa sababu kuna shilingi elfu 43 ninazolipa kila mwezi kwa mfumo wa afya wa SHA, na hilo pia tunahitaji kulijadili,” Sifuna ameandika.

Kadhalika ameendelea kuhoji kuhusu kodi ya PAYE ya shilingi laki tano ambayo anadai Rais hupokea kila mwezi, akidai kuwa fedha hizo hutumiwa katika matumizi ya chai na mandazi kwenye Ikulu.

Kauli ya Sifuna inajiri siku moja baada ya Rais Ruto kumkosoa kwa kupinga mpango wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu, akisema mpango huo umebuni fursa za ajira kwa maelfu ya vijana na unalenga kuboresha makazi ya familia zenye mapato ya chini.

Akizungumza Jumanne, Oktoba 13, 2026, Rais Ruto alihoji kwa nini Sifuna anapinga mpango ambao serikali inasema unabuni fursa za ajira kwa vijana.

“Sasa wewe na 1.8 million yako, watoto ya hawa watu wanakulipia hiyo mshahara, wewe hutaki hawa watoto ya hawa watu wapate kazi?” Rais aliuliza.

Mvutano huo unafuatia matamshi ya Sifuna katika bunge la Seneti mnamo siku ya Alhamisi, Oktoba 8, 2026 ambapo alitaja makato ya ushuru kwenye mshahara wake akitetea haki yake ya kuuliza serikali jinsi fedha zinazokusanywa kupitia ushuru wa nyumba zinavyotumiwa.

“Nilipokuwa nikikagua hati yangu ya mshahara, niligundua kuwa nimekuwa nikikatwa wastani wa shilingi elfu 24 kwa ajili ya ushuru wa nyumba,” Sifuna alisema.
Alisisitiza kuwa kuchangia katika mpango huo kunampa haki ya kuitaka serikali iwajibike kuhusu matumizi ya fedha hizo.

“Kama Mkenya anayekatwa ushuru nina haki kamili ya kuuliza maswali kuhusu jinsi fedha zinavyotumika,” alidokeza Sifuna.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here