Wakili wa Mahakama Kuu, Harrison Kinyanjui, amezua mjadala baada ya kutoa madai yanayotilia shaka uhusiano kati ya milipuko ya magonjwa kama vile Ebola na COVID-19 na maslahi ya wahisani wa kimataifa.
Kinyanjui amehoji nia ya ufadhili wa kimataifa na usambazaji wa vifaa tiba vinavyotolewa kwa nchi za Afrika kukabiliana na milipuko ya magonjwa, akidai kuwa huenda baadhi ya wahusika wananufaika na juhudi hizo.
“COVID-19 ilikuwa mradi wa Benki ya Dunia. Hii ndiyo sababu.” Wakili Kinyanjui amesema.
Kinyanjui pia ameibua maswali kuhusu hatua za kukabiliana na Ebola, akitaka kuchunguzwa kwa wanaonufaika na ufadhili na vifaa tiba vinavyotolewa wakati wa milipuko ya ugonjwa huo.
Wakili huyo ameendelea kudai kuwa Ebola inaweza kutumiwa kudhibiti idadi ya watu barani Afrika, akidai pia kuwa ugonjwa huo ni silaha ya kibayolojia.
Hata hivyo, hakutoa ushahidi wa kisayansi unaothibitisha madai hayo.
Madai hayo yanakinzana na maelezo ya kisayansi kuhusu jinsi Ebola inavyoenea. Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza kuwa maambukizi hutokea hasa kupitia kugusana moja kwa moja na damu au majimaji ya mwili ya mtu aliyeambukizwa ambaye tayari ana dalili.
Tofauti na magonjwa kama surua, Ebola haijulikani kuenea kwa urahisi kupitia hewa katika mazingira ya kawaida.
WHO inapendekeza hatua za kujikinga zinazojumuisha kuepuka kugusana na majimaji ya mwili ya watu walioambukizwa, kunawa mikono na kufuata mwongozo wa wahudumu wa afya.
Hatua hizo husaidia kupunguza hatari ya maambukizi, hasa katika maeneo yenye visa vilivyothibitishwa.
Kwa sasa, hakuna ushahidi wa kisayansi unaokubalika unaothibitisha madai kwamba Ebola iliundwa kama silaha ya kibaolojia kwa lengo la kudhibiti idadi ya watu barani Afrika.
Vilevile, madai kwamba COVID-19 ilikuwa mradi wa Benki ya Dunia hayajathibitishwa kwa ushahidi uliowasilishwa katika kauli hizo.









