Serikali imebaini kuwepo kwa makundi 109 ya uhalifu uliopangwa yanayofanya shughuli zake katika maeneo mbalimbali nchini, huku vyombo vya usalama vikiongeza juhudi za kudhibiti ghasia, vitisho na uhalifu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027.
Kwa mujibu wa Katibu wa Wizara ya Usalama wa Ndani Raymond Omollo, idadi hiyo imeongezeka kutoka makundi 89 yaliyotangazwa kuwa haramu mwaka 2016.
Serikali imeeleza wasiwasi kuhusu uwezekano wa makundi hayo kutumiwa kuwatisha wapiga kura, kuwashambulia wapinzani wa kisiasa au kuvuruga shughuli za kisiasa kuelekea uchaguzi ujao.
Kulingana na taarifa hiyo Eneo la Magharibi mwa Kenya lina idadi kubwa zaidi ya makundi hayo ikiwa na 38, ikifuatiwa na Eneo la Bonde la Ufa lenye makundi 22 na Nairobi yenye makundi 20.
Eneo la Nyanza lina makundi 12, Eneo la Pwani 11, Eneo la Mashariki matatu, Kaskazini Mashariki mawili, huku eneo la Kati likiwa na kundi moja.
“Vurugu, vitisho na matumizi ya makundi ya kihalifu kusukuma mbele maslahi ya kisiasa havina nafasi katika mchakato huo,” amesema Omollo.
Takwimu za serikali zinaonyesha kuwa kati ya Januari 1 na Agosti 31, 2026, Asasi za usalama ziliwakamata na kuwafikisha mahakamani washukiwa 1,827 kwa makosa yanayohusishwa na uhalifu uliopangwa na vitendo vya kihuni.
Kaunti ya Trans Nzoia ndiyo iliyorekodi idadi kubwa zaidi ya watu waliokamatwa, ikiwa na 491.
Katika kipindi hicho cha kati ya mwezi wa Januari na Agosti 2026, Asasi za usalama zilifanikiwa kuwapeleka Mahakamani na kuwahukumu watu 729 huku kesi 716 zikiendelea mahakamani
Kadhalika Kupitia operesheni zinazoongozwa na taarifa za kijasusi, wachunguzi wanawafuatilia viongozi wa makundi hayo pamoja na watu wanaowasajili wanachama na kuyafadhili.
Omollo amesema changamoto kubwa katika kupambana na makundi hayo ni muundo wao uliogatuliwa pamoja na kuenea kwa silaha ndogo hasa katika maeneo ya mipakani yaliyo katika hatari zaidi.
Wakati uo huo serikali imesema Asasi za usalama zitaendelea kuwa macho dhidi ya juhudi zozote za kuhamasisha makundi ya kihalifu kuvuruga shughuli za kisiasa au kusababisha ghasia wakati wa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027.
“Asasi za usalama zitaendelea kushika doria wakati wa shughuli za kisiasa na zitachukua hatua kwa mujibu wa sheria dhidi ya vitendo vya uhalifu, bila kujali anayehusika.” Amesema Duale.
Ameongeza kuwa watu wanaosajili, kufadhili au kuyaelekeza makundi hayo pia watawajibishwa pamoja na wale wanaotekeleza vitendo vya vurugu.









