Oparesheni ya usalama yawezesha kurudishwa kwa silaha haramu na kurejeshwa kwa mifugo Isiolo

0

Operesheni ya usalama katika Kaunti ya Isiolo imefanikiwa kupata silaha haramu 16 ndani ya wiki moja iliyopita, na kufanya jumla ya bunduki zilizopatikana kufikia 23 tangu operesheni hiyo ilipoanza wiki mbili zilizopita.

Maafisa wa usalama pia wamefanikiwa kuokoa mifugo 655 wakiwemo mbuzi na kondoo, na hivyo kuongeza idadi ya mifugo iliyorejeshwa hadi 2,389.

Aidha, ng’ombe 77 na ngamia mmoja pia walipatikana wakati wa operesheni hiyo.

Akizungumza katika Makao Makuu ya Polisi ya Kaunti ya Isiolo, Kamanda wa Polisi wa Kaunti hiyo Isaac Sang amesema silaha zote 23 zilipatikana ndani ya kaunti hiyo, huku operesheni ikiendelea pia katika kaunti jirani za Samburu na Laikipia.

“Silaha zote 23 zimepatikana ndani ya Kaunti ya Isiolo, ingawa operesheni bado inaendelea katika kaunti jirani za Samburu na Laikipia,” Sang alisema.

Ameongeza kuwa washukiwa sita wanazuiliwa na polisi kuhusiana na silaha hizo na wanasubiri kufikishwa mahakamani.

Kamanda huyo ametoa wito kwa yeyote aliye na silaha haramu kujisalimisha ili kunufaika na msamaha wa serikali, akionya kuwa watakaopatikana nazo watakabiliwa vikali na sheria.

“Tunatoa wito kwa yeyote aliye na silaha haramu ajisalimishe ili anufaike na msamaha wa serikali; atakayepatikana nazo atachukuliwa hatua kali za kisheria,” alionya.

Aidha, ameonya waendesha bodaboda dhidi ya kutumiwa kusafirisha dawa za kulevya kupitia njia za vichakani ili kukwepa ukaguzi wa barabarani, huku akihimiza ushirikiano kati ya wananchi na vyombo vya usalama ili kukomesha uhalifu.

“Baadhi ya wahalifu wanatumia pikipiki kusafirisha dawa za kulevya kupitia njia za vichakani, tunawataka waendesha bodaboda kukataa kutumiwa kwa uhalifu huo,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here