Shughuli za usafiri katika viwanja vya ndege nchini, ukiwamo ule wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, zimeendelea kutatizika kwa siku ya pili mfululizo kufuatia mgomo wa wafanyakazi wa viwanja vya ndege chini ya muungano wao wa KAWU.
Mamia ya wasafiri wamesalia kukwama kwenye viwanja hivyo huku safari nyingi za ndege zikicheleweshwa na zingine kusitishwa, hali inayozua taharuki kwa abiria wa wasafiri.
Baadhi ya wasafiri wameeleza kukerwa na hali hiyo wakisema hawajapewa taarifa za kutosha kuhusu lini huduma zitarejea kawaida.
Mgomo huo umeathiri pia usafirishaji wa mizigo na shughuli nyingine muhimu za kiuchumi zinazotegemea usafiri wa anga.
Haya yanajiri huku Waziri wa Utalii Rebecca Miano akitoa wito kwa wafanyakazi hao kurejea kazini haraka iwezekanavyo.
Akizungumza wakati wa kongamano la utalii jijini Nairobi, Miano amesema, iwapo mgomo huu utaendelea, sekta ya utalii itaathirika pakubwa kwa sababu watalii wengi hutegemea usafiri wa anga.
Ameongeza kuwa taswira ya Kenya kama kitovu cha utalii katika ukanda wa Afrika Mashariki inaweza kudhoofika ikiwa usumbufu huo utaendelea.
“Ni muhimu huduma zirudi kawaida haraka ili kulinda uchumi na sifa ya nchi yetu kimataifa.”
Wakati uo huo, ametoa wito kwa pande zote husika kuanza mazungumzo ya dharura ili kumaliza mgogoro huo.









