Mamlaka ya Kudhibiti Kawi na Petroli, EPRA, imeshusha bei ya dizeli kwa shilingi 5 kwa lita, huku bei ya petroli na mafuta ya taa ikisalia bila mabadiliko.
Kuanzia Agosti 15 hadi Septemba 14, petroli jijini Nairobi itauzwa kwa shilingi 214.03 kwa lita, dizeli ikishuka kutoka shilingi 222.86 hadi 217.86 kwa lita huku Mafuta ya taa yakiendelea kuuzwa kwa shilingi 191.38 kwa lita.
Jijini Mombasa, Super Petrol itauzwa kwa shilingi 210.87, dizeli shilingi 214.58, na mafuta ya taa shilingi 188.09 kwa lita.
Jijini Kisumu, Super Petrol itauzwa kwa shilingi 213.69, dizeli shilingi 218.08, na mafuta ya taa shilingi 191.63 kwa lita.
Katika taarifa yake Ijumaa Agosti 14, EPRA imesema marekebisho ya bei yanafuatia mapitio yake ya kila mwezi ya bei za mafuta chini ya Sheria ya Petroli, 2019, na Ilani ya Kisheria Nambari 192 ya 2022.
Bei ya petroli na mafuta ya taa imesalia bila mabadiliko kutokana na hatua za serikali za kudhibiti athari za kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la kimataifa.
Serikali imeongeza muda wa matumizi ya kodi ya thamani ya ziada (VAT) ya asilimia nane kwa bidhaa za petroli kwa miezi mitatu hadi Oktoba 14 mwaka huu.
Serikali pia imeidhinisha ruzuku ya shilingi milioni 945 kwa bei za mafuta katika miezi ya Julai na Agosti, kwa lengo la kuwalinda Wakenya dhidi ya ongezeko la bei za mafuta duniani.
Mapitio hayo yanajiri huku gharama ya bidhaa za mafuta zinazoagizwa kutoka nje zikionyesha mwelekeo tofauti.
EPRA imesema wastani wa gharama ya petroli iliongezeka kwa asilimia 6.99 kutoka dola 836.92 kwa kila mita ya ujazo mwezi Juni hadi dola 948.92 mwezi Julai.









