Marekani imetangaza ufadhili wa ziada wa dola milioni 242 kusaidia mwitikio wa haraka dhidi ya ugonjwa wa Ebola, maandalizi na juhudi za kibinadamu katika nchi zilizoathiriwa au zilizo katika hatari ya mlipuko huo Afrika Mashariki na Kati.
Fedha hizo zilitolewa wakati mamlaka za afya katika eneo lengwa zikiongeza ufuatiliaji, vipimo vya maabara, hatua za kuzuia na kudhibiti maambukizi kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Bundibugyo, aina ya ugonjwa wa Ebola, katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Uganda.
Marekani ilisema inaendelea kuwa mfadhili mkubwa zaidi wa kifedha wa mwitikio wa kimataifa dhidi ya Ebola, huku msaada wake ukilenga si tu kudhibiti maambukizi yaliyokuwa yakiendelea, bali pia kuimarisha mifumo ya afya katika nchi kama Kenya ambazo ziko hatarini kutokana na ukaribu wao na maeneo yaliyoathiriwa na nafasi yao kama vituo muhimu vya usafirishaji katika eneo.
Ufadhili huo mpya utasaidia shughuli za mwitikio wa dharura, ufuatiliaji wa magonjwa, vifaa vya matibabu, uwezo wa maabara, hatua za kuzuia na kudhibiti maambukizi, mawasiliano kuhusu hatari pamoja na hatua nyingine za maandalizi.
Kwa mujibu wa serikali ya Marekani, msaada wake hadi sasa umewezesha uchunguzi wa afya wa watu milioni 8.6 katika nchi zilizoathiriwa na zilizo katika hatari, na kuwafikia zaidi ya watu milioni moja kwa ujumbe wa kuelimisha kuhusu hatari ya Ebola.
Marekani pia imesaidia zaidi ya vituo 180 vya afya katika maeneo yaliyoathiriwa na Ebola na imeendesha moja kwa moja vituo 12 maalumu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa ajili ya kuwatenga na kuwatibu wagonjwa wa Ebola.
Takribani tani 300 za vifaa muhimu zimepatikana na kusambazwa chini ya mwitikio huo, ikiwa ni pamoja na vifaa vya kujikinga binafsi na bidhaa zinazohitajika kwa ajili ya maji, usafi wa mazingira, usafi wa mwili na kuzuia na kudhibiti maambukizi.
Kenya iliibuka kuwa sehemu muhimu ya mkakati wa maandalizi ya kikanda kutokana na kuwa na mtandao mpana wa usafiri wa anga na barabara unaoiunganisha na Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na nchi nyingine za eneo.
Serikali imetenga vituo maalumu vya kutenga na kutibu wagonjwa wa Ebola katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta, Hospitali ya Kitaifa ya Polisi na Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi, maeneo mengine ya mwitikio yakitambuliwa katika kaunti za mpakani zilizo katika hatari kubwa.
Marekani pia imehusika katika mipango ya kuanzisha kituo cha muda cha karantini ya Ebola katika kituo cha kijeshi cha Kenya katika Kaunti ya Laikipia kililenga hasa kuwahudumia wamarekani ambao huenda wakawa wameathiriwa na Ebola walipokuwa wakifanya kazi katika eneo hilo.
Kituo hicho kilichopendekezwa, ambacho kimeripotiwa kuwa na uwezo wa kuhudumia takribani vitanda 50, kilikumbwa na changamoto za kisheria na maandamano ya umma, huku wapinzani wakihoji makubaliano ambayo Kenya ingetumia kuwahifadhi raia wa Marekani ambao huenda walikuwa wameathiriwa na virusi hivyo.
Mahakama ya Kenya ilisimamisha mipango hiyo kwa muda, huku serikali ikiagizwa kutoa maelezo zaidi kuhusu kituo kilichopendekezwa.
Mwezi Juni 2026, waziri wa Afya Aden Duale alisema shughuli zilizohusiana na ujenzi katika eneo la Laikipia zilikuwa zimesitishwa kufuatia amri ya mahakama.









