Sifuna Akosoa Makubaliano ya Ruto na Sakaja, Asema Wakazi wa Nairobi Hawakushirikishwa.

0

Seneta wa kaunti ya Nairobi, Edwin Sifuna, sasa anaitaka serikali ya kitaifa pamoja na serikali ya kaunti ya Nairobi kusitisha makubaliano ya ushirikiano yaliyotiwa saini tarehe 17, February 2026, akilalamikia kutoshirikishwa kwa wakazi wa jiji.

Akizungumza na wanahabari, Sifuna amesema Makubaliano makubwa kama hayo yanapaswa kuwahusisha wakazi wa Nairobi akidokeza kuwa hawajashirikishwa kikamilifu na mchakato huu ni kinyume cha Katiba.

“Iwapo hatua hazitachukuliwa, nitaona ni vyema kupeleka kesi mahakamani kupinga mkataba huu. Wakazi wa Nairobi wanastahili kushauriwa kabla ya maamuzi makubwa kuchukuliwa.” Sifuna amesema.

Rais William Ruto mnamo tarehe  17, February 2026 alisisitiza kuwa serikali ya kitaifa haina mpango wa kutwaa uongozi wa kaunti ya Nairobi.

“Makubaliano haya ni kwa lengo la kuboresha huduma muhimu jijini kama maji, barabara, mifereji ya maji taka na makazi. Lengo letu ni kuhakikisha jiji kuu linaendeshwa vyema.” Kiongozi wa taifa alisisitiza.

Kwa upande wake Gavana wa Nairobi, Johnson Sakaja, alisema kuwa Makubaliano hayo ya ushirikiano yanazingatia maeneo manne muhimu yatakayowaboreshea maisha  wakazi wa jiji.

“Tunashirikiana na serikali ya kitaifa katika maeneo manne muhimu. Huu ni ushirikiano wa huduma kwa wananchi, sio kuhamisha majukumu yetu. Tumeweka wazi malengo ya kuboresha maisha ya Wakenya wa Nairobi,” Gavana Sakaja alihoji.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here