Ahmed Issack Hassan amejiuzulu rasmi kuwa mwenyekiti wa Mamlaka Huru ya Uangalizi wa Utendakazi wa Polisi (IPOA).
Hassan aliyeiongoza IPOA tangu mwaka wa 2024 alichukua hatua hiyo kufuatia kuapishwa kuwa jaji wa mahakama ya rufaa wiki tatu zilizopita.
Kwa mujibu wa taarifa za tume hiyo, Anne Mwangi aliyekuwa makamu mwenyekiti atakuwa akishikilia mikoba iliyoachwa kikaimu wakati mchakato wa kujaza nafasi hiyo ukiendelezwa kwa mujibu wa sheria.
Hassan aliyekuwa pia mwenyekiti wa zamani wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), alikuwa miongoni mwa majaji 14 walioteuliwa Januari 27 2026 baada ya kusailiwa na jopo la tume ya huduma za mahakama (JSC).
Wengine katika orodha hiyo ni wakili wa muda mrefu wa Rais William Ruto, Katwa Kigen, pamoja na Paul Lilan, Munyao Sila, Johnson Okoth Okello na Byram Ongaya.
IPOA ilianzishwa chini ya Sheria ya Mamlaka Huru ya Uangalizi wa Polisi ili kutoa usimamizi wa kiraia juu ya kazi za Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS).









