Kibagendi aonyeshwa mlango kwa kudhalilisha bunge

0

Mbunge wa Kitutu Chache Kusini Anthony Kibagendi amefurushwa bungeni kufuatia hatua ya kinidhamu iliyochukuliwa dhidi yake na spika wa bunge la kitaifa Moses Wetangula.

Katika kikao cha alasiri Jumanne tareh 17 2026, Wetangula alimpiga Kibagendi marufuku ya kuhudhuria vikao vya bunge au kuzuru maeneo ya bunge ikiwemo ofisi yake hadi pale ambapo angewasilisha ombi la msamaha kutokana na kile spika alitaja kuwa ni kulipaka tope jina la bunge kwa kudai lilikuwa limepigwa mnada na kugeuzwa kibaraka cha serikali tendaji.

Spika alielekeza kuwa mbunge huyo wa Kitutu Chache Kusini asiruhusiwe kuingia katika ukumbi wa Bunge, vikao vya kamati, wala ofisi yake ya bunge hadi atakapowasilisha “barua ya kuomba msamaha iliyoandikwa kwa lugha inayofaa” kwa Karani wa bunge ili ithibitishwe.

“Mheshimiwa Kibagendi, utaondolewa katika kikao cha bunge hili hadi ulete barua ya kuomba msamaha iliyoandikwa ipasavyo. Si kwangu, mimi nimezoea kusutwa, bali kwa bunge, kwa kuliletea fedheha,” aliamua Wetang’ula.

“Barua hiyo iwasilishwe kwa karani. Itachunguzwa kwa makini. Ikiwa maneno yake yatakubalika, italetwa bungeni na utaruhusiwa kurejea. Kwa sasa, umeondolewa katika shughuli za bunge hili, maeneo ya bunge, vikao vya kamati, pamoja na ofisi yako.”

Hoja hiyo iliibuliwa kupitia hoja ya nidhamu na mbunge wa Laikipia Kaskazini, Sara Korere, ambaye alimlaumu Kibagendi kwa madai ya kutoa matamshi ya kudhalilisha spika na uongozi wa bunge wakati wa kipindi cha mahojiano ya asubuhi kwenye runinga moja nchini.

“Ofisi ya spika inawakilisha mamlaka na hadhi ya bunge hili tukufu,” alisema Korere.

“Shambulizi dhidi ya ofisi ya spika si shambulizi kwako tu, mheshimiwa spika, bali ni shambulizi kwa bunge hili lenyewe.”

Kwa upande wake, Kiongozi wa Wengi, Kimani Ichung’wah, aliunga mkono uamuzi wa spika akirejelea kanuni ya 107 kuhusu mwenendo usiofaa akisema mbunge hufanya kosa la utovu wa nidhamu anapotoa madai bila uthibitisho wa kutosha.

Wetang’ula alitumia fursa hiyo kukanusha madai kwamba bunge lilikuwa likifanya kazi kwa kuegemea serikali tendaji, akitetea uhuru wa ofisi yake.

“Spika wa bunge hili hana kura. Spika hashiriki mjadala. Spika haanzishi mjadala. Spika hawasilishi hoja wala mswada wowote katika Bunge hili,” alisema.

Spika aliwataka wabunge kuwa na tahadhari wanapozungumza kwenye majukwaa ya umma, akionya kuwa kauli zao zinaakisi taasisi nzima.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here