Kikosi maalum kubuniwa ili kuimarisha usalama wa jiji kuu

0

Rais William Ruto ameagiza kubuniwa kikosi maalum cha polisi kuhudumu jijini Nairobi (Metropolitan) ili kuimarisha usalama ndani ya kaunti hiyo.

Akizunguma Juma nne tarehe 17 Februari 2026 wakati wa kusaini makubaliano ya ushirikiano kati ya serikali ya kaunti ya Nairobi na serikali ya kitaifa katika ikulu, rais Ruto alimwelekeza waziri wa Mambo ya Ndani, Kipchumba Murkomen, kuandaa mfumo wa utekelezaji ndani ya siku 60 kwa ajili ya kikosi hicho cha polisi.

Kwa mujibu wa rais, hatua hiyo ililenga kulifanya jiji kuu kuwa kitovu salama kwa wananchi pamoja na wawekezaji.

“Usalama hauwezi kujadiliwa katika jiji kuu la kisasa kama Nairobi. Hivyo basi, namwagiza waziri wa Mambo ya Ndani kuandaa na kuwasilisha, ndani ya siku 60, mfumo wa kuanzisha kikosi maalum cha polisi wa Nairobi Metropolitan. Tutaifanya Nairobi kuwa salama kwa wananchi, wageni, wawekezaji na wafanyibiashara kwa ujumla,” rais alisema.

Kiongozi huyo wa taifa aliwahakikishia wananchi kwamba makubaliano hayo mapya ya ushirikiano yangeibadilisha Nairobi kufikia viwango vya kimataifa.

“Kwa ujumla wake, hatua hizi zilizoimarishwa za ushirikiano zitaifanya Nairobi iwe bora zaidi kuishi, salama zaidi na yenye ufanisi zaidi. Aidha, zitainua hadhi yake,” alisema.

“Kwa vitendo, hii inamaanisha barabara salama zaidi, mwangaza bora, maji ya uhakika, usafi ulioboreshwa, mifumo imara ya usafiri, mifumo ya kisasa ya usimamizi wa taka, na kuimarishwa kwa usalama wa mijini.”

Aidha, alisisitiza mipango ya kujenga uwanja mpya wa ndege wa kiwango cha kimataifa mwaka 2026 kupitia mfumo wa ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), akisema kuwa hatua hiyo ingefungua taifa la Kenya kwa uwekezaji na utalii wa kimataifa.

Kwa ujumla, Rais Ruto alibainisha kuwa ushirikiano wa shilingi bilioni 80 ungeimarisha na kuhuisha sura ya jiji kuu.

Hayo yalijiri kufuatia ripoti ya Jukwaa la Usalama kutoka kwa wizara ya Mambo ya Ndani iliyofichua kuwa zaidi ya magenge 130 yalikuwa yakitishia usalama jijini.

Sehemu ya mapendekezo ya ripoti hiyo ilihusisha kupelekwa kwa vikosi maalum zaidi ili kushughulikia changamoto za kipekee katika maeneo mbalimbali nchini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here