Mamlaka ya Kitaifa ya Kupambana na Matumizi ya Pombe na Dawa za Kulevya (NACADA) inashirikiana na viongozi wa kidini ili kutumia ushawishi wao katika ukuzaji wa maadili na mwongozo kwa vijana huku pia ikitekeleza sera maalum katika shule, maeneo ya kazi na mitaa.
Haya ni kwa mujibu wa mwenyekiti wake askofu Dkt. Stephen Mairori, akitoa wito wa kuimarishwa kwa juhudi zinazoongozwa na jamii katika kuzuia matumizi ya dawa za kulevya, akionya kuwa kuongezeka kwa matumizi yake miongoni mwa vijana kunahatarisha mustakabali wa taifa la Kenya.
“Mkakati wetu unaleta uwiano kati ya kupunguza upatikanaji na kupunguza mahitaji, kwa sababu mustakabali salama unahitaji kuvunja njia za upatikanaji na pia kuimarisha azma ya kukataa,” aliongeza.
Akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa warsha ya wiki ya kitaifa ya kuzuia matumizi ya dawa za kulevya iliyofanyika katika shule ya mafunzo ya uongozi siku ya Alhamisi tarehe 12 Februari 2026, Dkt. Mairori alisisitiza kuwa kinga ilipaswa kubaki kuwa kipaumbele cha kitaifa kinachojikita katika familia, taasisi za kidini, shule na maeneo ya kazi.
Alibainisha kuwa ingawa matumizi ya dawa za kulevya bado ilikuwa ni changamoto, idadi kubwa ya wakenya walichagua kutozitumia, akirejelea takwimu za NACADA zilizoonyesha kuwa asilimia 42.5 ya wakenya hawajawahi kutumia dawa za kulevya maishani mwao.
Hata hivyo, mwenyekiti huyo alieleza wasiwasi kuhusu matumizi ya dawa za kulevya miongoni mwa vijana, akifichua kuwa asilimia 17.5 ya watu wazima na asilimia 26.6 ya wanafunzi wa vyuo vikuu wamewahi kutumia dawa za kulevya, hali iliyoashiria haja ya dharura ya hatua mahususi katika taasisi za elimu.
“Kenya ni taifa la vijana, na kundi letu muhimu zaidi liko hatarini. Upatikanaji wa dawa za kulevya, hasa karibu na taasisi zetu za elimu, ni janga tunalopaswa kukabiliana nalo kwa umoja na haraka,” alisema.
Dkt. Mairori alieleza mkakati wa pande mbili uliolenga kuimarisha juhudi za kinga ambazo tayari zilikua zikifanya kazi katika kiwango cha mashinani, pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya serikali, jamii na wadau wengine ili kuziba pengo kati ya sera na utekelezaji.
Mwenyekiti huyo pia aliwatambua watu walioko katika hatua ya kupona, akiwataja kama ushahidi hai kwamba mabadiliko yanawezekana, akiwahimiza kushiriki uzoefu wao ili kuwatia moyo wengine wanaopambana na uraibu.
Kaulimbiu ya Wiki ya Kinga ya mwaka 2026 ilikuwa “Jamii Zilizowezeshwa, Mustakabali Bora,” ikisisitiza jukumu la uwajibikaji wa pamoja katika kushughulikia matumizi ya dawa za kulevya na kujenga jamii zenye afya bora.









