Mfanyibiashara alipwa 3.5M kwa kufurushwa nchini kinyume cha sheria.

0

Mahakama kuu imeamuru serikali ya Kenya kumlipa mfanyibiashara Abdiqiadar Omar Osman fidia ya shilingi milioni 3.5 kwa kumfurusha kutoka nchini hadi taifa la Somalia bila kufuata taratibu za kisheria.

Kulingana na uamuzi wa mahakama uliotolewa na jaji Bahati Mwamuye, Osman alibainika kuwa raia wa Kenya kwa kuzaliwa na kwamba hatua zilizochukuliwa dhidi yake zilikuwa kinyume na sheria na ukiukaji mkubwa wa katiba.

Jaji Mwamuye alieleza kwamba kukamatwa kwa Osman Mei, 2018 alipokuwa akisafiri kutoka nchini Uganda hadi Kenya kulikiuka haki zake zakikatiba.

Kupitia wakili Danstan Omar Mahakama ilifahamishwa kwamba mhusika hakupewa sababu za kukamatwa kwake, alinyimwa fursa ya kusaka wakili na kukosa kufikishwa mahakamani katika kipindi cha saa 24 ilivyotakiwa chini ya kifungu cha 49 cha Katiba.

Badala yake ilisemekana kwamba alipelekwa kwenye ofisi za uhamiaji kwenye jengo la Nyayo jijini Nairobi na kuondolewa nchini kwenda Somalia bila mchakato wowote wa kisheria au amri halali.

Mahakama ilibaini pia kwamba Osman alikuwa na cheti cha kuzaliwa nchini sawa na kitambulisho cha kitaifa kudhibitisha uraia wake.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here