Ufisadi wasalia donda nchini, ripoti yabaini.

0

Ripoti ya shirika la Transparency international ya mwaka wa 2025 kuhusu ufisadi imetaja Kenya kuwa miongoni mwa mataifa yanayokumbwa na viwango vya juu vya visa hivyo sawa na juhudi finyu za kuukabili.

Ripoti hiyo iliyotolewa Jumanne tarehe 10 Februari 2026 imeonyesha kuwa alama ya Kenya ilishuka hadi 30 kati ya 100 ikilinganishwa na 32 mwaka uliotangulia wa 2024 ikiorodheshwa ya 130 kati ya 181 katika mataifa ambayo ufisadi umesalia kuwa tishio.

Kulingana na ripoti ya shirika hilo Kenya iliorodheshwa nyuma ya Rwanda na Tanzania zilizoshikilia nafasi ya 58 na 40, mtawalia kutoka ukanda wa Afrika Mashariki.

Rwanda ambayo ilitajwa kuwa taifa lenye visa vichache vya ufisadi katika ukanda wa Afrika Mashariki, ilikuwa imeonyesha dalili za kupiga hatua kuanzia mwaka wa 2024, huku Tanzania ikitajwa kama iliyolegea hatua moja nyuma kutoka mwaka wa 2024.

Mbali na Kenya kutajwa kama inayokabiliwa na ufisadi, Uganda na DR Congo yalitajwa kurekodi viwango vya juu vya ufisadi huku Burundi, Somalia na Sudan Kusini, yakionekana kuwa katika hali tete ya ufisadi.

Katika ripoti yake shirika hilo lilitaja matumizi mabaya ya mamlaka kuwa kichocheo kikuu cha ufisadi

‘‘Katika wakati ambapo tunashuhudia hatari ya kupuuzwa kwa kanuni za kimataifa kutoka kwa baadhi ya nchi, tunatoa wito kwa serikali na viongozi kutenda kwa uadilifu na kutimiza wajibu wao wa kuhakikisha mustakabali bora kwa watu kote ulimwenguni,’’ alisema François Valérian, mwenyekiti wa Transparency International.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here