Chama cha Orange Democratic Movement ODM kupitia kamati kuu ya kitaifa (NEC) kimembandua Edwin Sifuna kutoka kwenye wadhifa wa katibu mkuu.
Uamuzi wa kumwonyesha Sifuna mlango uliafikiwa katika mkutano wa kamati kuu ya chama uliofanyika jijini Mombasa Jumatano tarehe 11 Februari 2026 chini ya uongozi wa kinara wa chama Oburu Oginga ukihusishwa na masuala kadhaa yakiwamo utovu wa nidhamu na ukiukaji wa kanuni za chama.
Nafasi ya Sifuna ilitangazwa kuchukuliwa kikaimu na aliyekuwa naibu wake ambaye pia ni mbunge wa kaunti ya Busia Catherine Omanyo hadi pale uchaguzi utakapofanywa kuijaza rasmi.
“Kamati kuu ya kitaifa ilieleza kutatizika na ongezeko la viwango vya ukosefu wa nidhamu ndani ya chama haswa katika kiwango cha uongozi. Kamati ilisisitiza kuwa ODM inaongozwa na Katiba ya chama, utawala wa kisheria sawa na uamuzi wa pamoja kupitia vitengo vyake vilivyobuniwa kihalali,’’ chama kilieleza kupitia taarifa iliyosomwa na Omanyo.
‘‘Baada ya kujadili masuala yanayohusu mwenendo wa Katibu mkuu Edwin Sifuna, NEC iliazimia kumwondoa madarakani mara moja kwa mujibu wa katiba ya chama na sheria husika. Kwa hivyo, naibu katibu mkuu Catherine Omanyo atakaimu katika wadhifa huo hadi atakapochaguliwa atakayechukua rasmi nafasi hiyo.’’
Kando na mabadiliko katika uongozi wa chama, kamati hiyo vilevile iliidhinisha maamuzi yaliyoafikiwa na kamati kuu iliyohusisha kumjukumu Oburu kuongoza mazungumzo ya ushirikiano wa chama cha chungwa na vyama vingine kuelekea uchaguzi mkuu ujao.
Kando na Sifuna, baadhi ya wanachama wengine wa kamati kuu ambao wamefurushwa ni pamoja na mbunge wa Saboti Caleb Amisi, seneta wa Taita Taveta Jones Mwaruma na aliyekuwa diwani Kipkorir Menjo.









