Mvutano kati ya Maseneta na Magavana wazidi kuchacha kuhusu vikao vya kamati ya uhasibu

0

 

Mvutano kati ya Seneti na Baraza la Magavana umeendelea kushika kasi huku wanachama wa Kamati ya Uhasibu wa Fedha za Umma wakijibu madai ya magavana kwamba wanadhalilishwa wanapofika mbele ya kamati hiyo, na hata wakati mwingine kudai kuitishwa hongo.

Kamati hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Seneta wa Homa Bay Moses Kajwang, imepuzilia mbali madai hayo ikisema kuwa inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa kanuni za Bunge na Katiba.

Kajwang amesisitiza kuwa jukumu la kamati hiyo ni kuhakikisha uwajibikaji katika matumizi ya fedha na rasilimali za umma, akiongeza kuwa magavana wanapaswa kujiandaa ipasavyo wanapoitwa kufafanua masuala ya kifedha kwa niaba ya wananchi.

Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna kwa upande wake alikosoa vitisho vya baadhi ya magavana kwamba watasusia vikao hivyo, akisema hatua hiyo inaashiria uongozi dhaifu katika kaunti.

“Tunazungumziwa katika hoteli za Mombasa na watu wanaojiita Waheshimiwa, ilhali hakuna lolote la kuheshimiwa katika mienendo yao.” Sifuna alisema

Aliongeza kuwa baadhi ya magavana hujitokeza mbele ya kamati bila maandalizi na bila nyaraka sahihi za kifedha, huku wengine wakishindwa kufafanua stakabadhi wanazowasilisha wao wenyewe.

Kwa upande wake, Seneta wa Nandi Samson Cherargei alisema baadhi ya magavana wanakwepa vikao vya kamati hiyo kwa sababu wanahusishwa na madai ya ufisadi.

Spika wa bunge la Seneti, Amason Kingi, aliunga mkono kamati hiyo akisema Seneti haitayumbishwa katika kutekeleza jukumu lake la kikatiba la kusimamia matumizi ya fedha za umma.

“Seneti haitayumbishwa wala kuzuiwa na shinikizo lolote katika kutekeleza wajibu wake wa kikatiba wa kuhakikisha uwajibikaji na usimamizi wa matumizi ya fedha za umma kwa mujibu wa Kifungu cha 229 cha Katiba.” Kingi alisema

Kauli hizi zinajiri huku magavana wakishikilia msimamo wao kwamba hawatajitokeza mbele ya kamati hiyo hadi malalamishi yao yaangaziwe kupitia mazungumzo rasmi kati ya Baraza la Magavana na Seneti.

“Hatutajitokeza mbele ya kamati hii hadi malalamishi yetu yote ya udhalilishaji na vitendo vya hongo yashughulikiwe kupitia mazungumzo rasmi na Seneti.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here