Rais William Ruto ameondoa hofu kuhusu uwezekano wa kuingiliwa kisiasa kwa Hazina ya Kitaifa ya Miundombinu na Hazina ya Utajiri wa Taifa, akisisitiza kuwa watu walioteuliwa kisiasa hawataruhusiwa kusimamia au kuongoza taasisi hizo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa jukwaa la Safaricom Ziidi Trader katika Soko la Hisa la Nairobi (NSE), Rais Ruto amesema serikali itaweka mifumo madhubuti ya uongozi ili kulinda hazina hizo dhidi ya ushawishi wa kisiasa.
“Hatutaruhusu watu wenye misimamo au uteuzi wa kisiasa kuendesha hazina hizi. Tunajenga mifumo itakayohakikisha uwajibikaji, uwazi na ufanisi,” alisema Rais Ruto.
Rais alifafanua kuwa miongoni mwa hatua zitakazotekelezwa ni kuweka sharti la kipindi cha miaka mitano kwa mtu yeyote aliyewahi kufanya kazi katika sekta ya umma kabla ya kuteuliwa katika bodi za taasisi hizo, hatua inayolenga kuimarisha uhuru na weledi wa uongozi.
“Hili ni jukwaa litakalowezesha wananchi wengi zaidi, hususan vijana na wanawake, kushiriki katika uwekezaji na kukuza ujumuishaji wa kifedha,” aliongeza.
Rais pia ameendelea kusisitiza kuwa uchumi wa Kenya unaendelea kuimarika, akibainisha kuwa serikali inalenga kukusanya shilingi trilioni tano kwa ajili ya maendeleo ya kitaifa bila kuwaongezea Wakenya mzigo wa kodi au kuongeza madeni ya taifa.
Kwa mujibu wa Rais, Soko la Hisa la Nairobi litakuwa kitovu cha mpango huo kupitia uuzaji wa hisa za mashirika ya umma, hatua inayolenga kupata mtaji wa maendeleo na kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika ukuaji wa uchumi.









