Mamlaka ya Kuangazia Utendakazi wa Maafisa wa Polisi (IPOA) imeanzisha uchunguzi kuhusu tukio la kuuliwa kwa kupigwa risasi kwa mwanafunzi mwenye umri wa miaka 21 katika eneo la Huruma, jijini Nairobi.
Katika taarifa yake, Naibu mwenyekiti wa IPOA Ann Wanjiku amesema kuwa maafisa wake wametumwa katika eneo la tukio ili kufanya uchunguzi wa kina kuhusu mazingira yaliyosababisha kifo hicho.
“Mnamo Jumapili, Februari 8, 2026, IPOA ilituma maafisa wake kutoka Ofisi ya Mkoa wa Nairobi kuanza uchunguzi kuhusu tukio la kupigwa risasi lililotokea jioni ya Februari 7, 2026 katika eneo la Huruma, Kaunti ya Nairobi,” Wanjiku alisema.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, mwanafunzi huyo, aliyefahamika kwa jina Cheryl Adhiambo, aliuawa mnamo Februari 7, 2026 wakati wa oparesheni ya polisi ya kuwasaka washukiwa wa wizi katika eneo hilo.
Maafisa wa IPOA wanasema wanalenga kukusanya ushahidi, kurekodi kauli za mashahidi na kuchambua vielelezo mbalimbali ili kubaini iwapo matumizi ya nguvu yaliyotumika yalikuwa ya kisheria na kufuata taratibu zinazohitajika.
“Uchunguzi unaendelea, huku wachunguzi wetu wakiendelea kukusanya ushahidi, kuwahoji mashahidi, na kuchambua sampuli pamoja na vielelezo vilivyopatikana. “
Mamlaka hiyo imesema lengo ni kubaini mazingira yaliyosababisha tukio la kupigwa risasi ili kutoa mapendekezo kwa taasisi husika.
IPOA imesema itatoa taarifa zaidi pindi uchunguzi utakapokamilika.
Cheryl ambaye alikuwa amemaliza mtihani wake wa mwaka wa kwanza alikuwa amerejea nyumbani ili kumsaidia mamaye kwenye kibanda chao cha kuuza samaki alipopigwa risasi kichwani na maafisa wa polisi waliokuwa wakimfukuza mshukiwa wa wizi katika mtaa huo.









