Mahakama ya Rufaa imebatilisha uamuzi wa Mahakama Kuu uliokuwa umeamuru kuwa Hazina ya Kitaifa ya Ustawishaji wa Maeneo Bunge (NGCDF) si halali kikatiba.
Katika uamuzi wake, Mahakama ya Rufaa imesema Mahakama Kuu ilifanya makosa ya kisheria katika kufutilia mbali uhalali wa hazina hiyo.
Jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa wakiongozwa na Jaji Daniel Musinga, Jaji Francis Tuiyott, na Jaji Aggrey Muchelule wametengua hukumu iliyotolewa mnamo Septemba 20, 2024, wakisema kuwa marekebisho yaliyofanywa kwenye Sheria ya NGCDF mnamo mwaka 2022 na 2023 hayakufanya ombi la awali lililokuwa limewasilishwa dhidi ya hazina hiyo kuwa batili.
Mahakama imeeleza kuwa Sheria ya Hazina ya Kitaifa ya NGCDF haikiuki kanuni wala muundo wa kikatiba wa mfumo wa ugatuzi.
Aidha, majaji wamebaini kuwa hazina hiyo haiingilii mgawanyo wa majukumu kati ya serikali ya kitaifa na serikali za kaunti, kinyume na ilivyokuwa imebainishwa katika uamuzi wa awali wa Mahakama Kuu.
“Kinyume na uamuzi wa Mahakama Kuu, Sheria ya hazina ya NGCDF, 2015 haikiuki kanuni na muundo wa ugatuzi, wa majukumu kati ya serikali ya kitaifa na ya kaunti,” majaji waliamua.
Uamuzi huo wa Mahakama ya Rufaa sasa unaipa NGCDF mwanya wa kuendelea kutekeleza majukumu yake huku mjadala kuhusu uendeshaji wake ukiendelea katika majukwaa ya kisiasa na kisheria.









