IEBC yateua mridhi wa afisa mtendaji Hussein Marjan

0

Tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC) imemteua Moses Ledama Sunkuli kuwa kaimu afisa mkuu mtendaji (CEO) ambaye pia atahudumu kama karani wa tume.

Kupitia taarifa iliyotiwa saini na mwenyekiti Erastus Ethekon Alhamisi tahere 5 Februari 2026, IEBC ilieleza kwamba Sunkuli ambaye alikuwa mkurugenzi mkuu wa operesheni za uchaguzi wa tume wakati wa uteuzi wake, ataongoza katika nafasi hiyo kwa muda wa miezi sita au hadi wakati ambapo mchakato wa kumpata atakayeijaza nafasi hiyo utakapokamilika.

Nafasi hiyo ilisalia wazi baada ya Marjan Hussein Marjan kujiuzulu kutokana na kile tume ilidai kuwa ni makubaliano ya kufanya hivyo.

Ethekon alitumia fursa hiyo kutambua na kushukuru mchango wa Marjan tangu alipoteuliwa mwezi Machi mwaka wa 2022 akitambua uongozi wake haswa wakati ambapo tume ilihudumu pasipo na idadi kamili ya makamishna.

“Tunamshukuru Marjan kwa kujitolea kwake sawa na huduma yake ya kitaalamu kwa IEBC na tunamtakia mema katika majukumu yake ya baadaye,” Ethekon aliongeza.

Muda wa kuhudumu kwa Marjan ulitarajiwa kukamilika mwezi Machi mwaka wa 2027 ambapo ingekuwa ni miezi mitatu tuu kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti, Ethekon akitaja hatua ya Marjan kama iliyotoa nafasi ya kutosha ya kutekeleza mchakato wa kumpata mridhi wake kabla ya uchaguzi huo.

Marjan alijiuzulu Jumanne tarehe 3 Februari 2025 siku chache baada ya kile kilichoonekana kuwa msukumo kutoka kwa muungano wa upinzani uliolalamikia kuwepo kwake ofisini kuelekea uchaguzi mkuu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here