IEBC yawinda gen z kupitia usajili wa kidijitali

0

Tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC) imetangaza mpango wa kuzindua jukwaa la kidijitali litakalosaidia kurahisisha usajili wa wapiga kura kama njia ya kufikia idadi lengwa ya wapiga kura milioni 6.3 wapya.

Katika hafla ya maombi Jumatano tarehe 4 Februari, mwenyekiti wa IEBC Erustus Ethekon alisema kwamba jukwaa hilo litawawezesha wanaojisajili kujaza taarifa na stakabadhi zao kupitia njia ya mtandao.

‘‘Tunazindua jukwaa la kidijitali ambapo ukiwa na kiunganishi, fomu ya kabla ya usajili, unaweza ukajaza maelezo yako yote kisha utakachohitajika kufanya ni kutembelea kituo cha huduma au cha usajili wa wapiga kura kilicho karibu ilia lama zako za vidole zichukuliwe,’’ alisema Ethekon.

Mwenyekiti huyo wa IEBC alisisitiza kuwa usajili wa wapiga kura ni mojawapo ya ajenda kuu ya tume kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 zoezi ambalo litawalenga waliohitimu umri wa miaka 18, wale ambao hawakuwa wamejisajili sawa na walionuia kubadilisha kituo cha kupigia kura.

Alisema licha ya awamu ya kwanza ya usajili kurekodi jumla ya wapiga kura 200,000 wapya iliyoonekana kuwa idadi ya chini, tume haitalegeza kamba katika kuendeleza kampeni za uhamasisho.

‘‘Hatuna wasiwasi kuhusu idadi ya chini. Usajili endelevu upo katika maeneo bunge. Mpango wetu ni kuanzisha zoezi la jumla la usajili mwezi Machi na kutokana na hilo tutabuni vituo vya usajili katika kila Kijiji,’’ aliongeza.

Katika hafla hiyo IEBC iliwahimiza washikadau kuchangia katika kuufanya uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2027 kuwa bora zaidi katika historia ya taifa la Kenya.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here