Waziri Mudavadi asema Kenya Haiegemei Upande Wowote kwenye vita vya Mashariki ya Kati

0

Serikali imesisitiza kuwa inaendelea kuzingatia usalama wa Wakenya wanaoishi katika eneo la Mashariki ya Kati huku pia kukiwa na wito kwa serikali kutoongeza bei ya mafuta nchini.

Waziri mwenye mamlaka makuu Musalia Mudavadi amesema serikali inafuatilia kwa karibu usalama wa zaidi ya Wakenya nusu milioni wanaoishi, kufanya kazi na kusoma katika mataifa ya Mashariki ya Kati.

Akizungumza jijini London, Uingereza, Mudavadi amesema Kenya inaendelea kushikilia msimamo wa kutokuwa upande wowote katika mzozo unaoendelea katika eneo hilo, huku ikisisitiza umuhimu wa amani na kufuata sheria za kimataifa.

“Kenya haijaegemea upande wowote katika mzozo wa Mashariki ya Kati; imeendelea kutoa wito wa kupunguzwa kwa mvutano, mazungumzo na kuheshimiwa kwa sheria za kimataifa,” Mudavadi alisema.

Hata hivyo, huku mvutano huo ukiendelea, onyo limetolewa kwa serikali dhidi ya kuongeza bei ya mafuta nchini.

Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro ameonya kuwa Wakenya hawapaswi kubebeshwa mzigo wa kupanda kwa gharama ya mafuta kwa kisingizio cha mabadiliko ya soko la kimataifa.

Akizungumza katika soko la Kahuro kaunti ya Murang’a, Nyoro alidai kuwa kuna juhudi za kushinikiza Mamlaka ya Kudhibiti Kawi (EPRA) kuongeza bei ya mafuta licha ya hali ya sasa ya soko.

“Wakenya hatutarajii EPRA ianze kuwahadaa wananchi kwa kuongeza bei ya mafuta, kwa sababu mafuta yaliyopo sokoni kuanzia Machi hadi Aprili yaliingizwa nchini kabla bei ya mafuta duniani kuanza kupanda. Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita serikali pia iliongeza ushuru wa mafuta kutoka asilimia 8 hadi asilimia 16,” Nyoro alisema.

Nyoro ameongeza kuwa serikali inapaswa kuwa makini katika maamuzi yake ili kuhakikisha wananchi hawalemewi zaidi na gharama za maisha zinazozidi kuongezeka.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here