Uchumi wa Kenya unatarajiwa kuimarika na kukua kwa asilimia 5.3 mwaka 2026, ikilinganishwa na asilimia 4.7 mwaka 2024, huku serikali ikiendelea kutekeleza mikakati ya kuimarisha uthabiti wa uchumi, kukuza sekta muhimu na kuongeza ukusanyaji wa mapato ya serikali.
Akizungumza kuhusu mwelekeo wa uchumi, John Mbadi ambaye ni waziri wa fedha amesema serikali inapendekeza bajeti ya shilingi trilioni 4.7 katika mwaka wa kifedha wa 2026/2027.
Katika bajeti hiyo, shilingi trilioni 3.45 zimetengwa kwa matumizi ya kawaida ya serikali huku shilingi bilioni 749.5 zikielekezwa katika miradi ya maendeleo.
“Serikali inalenga kuhakikisha uchumi unaendelea kukua kwa njia endelevu kupitia uwekezaji katika sekta muhimu na kuboresha ukusanyaji wa mapato,” alisema Mbadi.
Aidha, serikali za kaunti zinatarajiwa kupokea shilingi bilioni 495.5 ili kugharamia utoaji wa huduma chini ya mfumo wa ugatuzi.
Hata hivyo, Mbadi ameonya kuwa ongezeko la gharama za mishahara serikalini linaendelea kuwa changamoto kubwa kwa uchumi wa taifa. Kwa mujibu wake, gharama hizo zinakadiriwa kufikia takriban shilingi trilioni 3.5 ya matumizi ya kawaida ya serikali, hali ambayo inaweza kuhatarisha uthabiti wa kifedha wa nchi.
“Gharama za mishahara serikalini zinaendelea kuongezeka na hii ni changamoto inayohitaji hatua za haraka ili kuhakikisha uthabiti wa kifedha wa taifa,” aliongeza.
Ili kukabiliana na hali hiyo, serikali inapanga kuendelea kutekeleza sera za kubana matumizi, kuboresha ukusanyaji wa mapato, kufanya mageuzi ya kiutawala na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.
Mbadi pia amependekeza uwezekano wa marekebisho ya katiba ili kupunguza kujirudia kwa majukumu kati ya serikali ya kitaifa na zile za kaunti. Kulingana naye, gharama za mishahara katika serikali za kaunti zimeongezeka kutoka shilingi bilioni 75 hadi shilingi bilioni 90, hali inayotokana na kuongezeka kwa idadi ya nyadhifa za uongozi.
Kwa mujibu wa Wizara ya Fedha, mfumo wa bajeti pia unajumuisha hazina ya dharura ya shilingi bilioni 2 na nakisi ya bajeti inayokadiriwa kufikia shilingi trilioni 1.1. Nakisi hiyo inapangwa kufadhiliwa kupitia mikopo ya nje ya shilingi bilioni 225.5 na mikopo ya ndani ya shilingi bilioni 890.4.
Mbadi pia amekiri kuwa serikali inakabiliwa na changamoto katika ukusanyaji wa mapato, akibainisha kuwa makadirio ya mapato mara nyingi yamekuwa yakizidishwa kuliko uhalisia.
“Ni muhimu kuweka makadirio ya mapato yanayoendana na hali halisi ya uchumi ili kuepuka changamoto katika utekelezaji wa bajeti,” alisema.
Hata hivyo, serikali inalenga kukusanya shilingi trilioni 3.588, sawa na asilimia 17.1 ya pato la taifa, kupitia mageuzi ya mfumo wa kodi pamoja na matumizi ya teknolojia katika ukusanyaji wa mapato.









