Waziri wa Barabara na Uchukuzi Davis Chirchir amekanusha madai kwamba zabuni ya upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) imetolewa kwa kampuni moja ya China.
Hii ni baada ya ripoti za baadhi ya vyombo vya habari nchini zilizodai kuwa kampuni ya China Road and Bridge Corporation (CRBC) ilikuwa imeshinda zabuni hiyo, kwa ushirikiano na kampuni ya IMC Construction Kenya inayodaiwa kuhusishwa na mfanyabiashara Wicknell Chivayo wa Zimbabwe.
Hata hivyo, Chirchir amepuuzilia mbali madai hayo akisema kampuni zilizotajwa hazikuwahi kuwasilisha maombi ya kushiriki katika zabuni hiyo, na hivyo haziko katika orodha ya wakandarasi waliowasilisha mapendekezo yao.
“Kampuni zilizotajwa katika ripoti za vyombo vya habari hazikutuma maombi na si sehemu ya wanakandarasi waliowasilisha maombi,” amesema Chirchir.
Pia amekanusha madai kuhusu gharama ya mradi huo, akifafanua kuwa upanuzi wa JKIA unakadiriwa kugharimu takriban shilingi bilioni 154, na si bilioni 375 kama ilivyoripotiwa awali.
“Mradi huu unakadiriwa kugharimu takriban shilingi bilioni 154 na wala siyo bilioni 375 kama ilivyodaiwa katika vyombo vya habari,” ameongeza.
Aidha, amesema baadhi ya taarifa zilizoripotiwa kwenye vyombo vya habari si sahihi na zimechangia kuleta mkanganyiko kuhusu mchakato mzima wa mradi huo.
Sakata hiyo ya zabuni ya JKIA imeendelea kuzua mjadala nchini, ikikumbukwa kuwa si mara ya kwanza kwa mradi huo kuingia kwenye utata.
Mwishoni mwa mwaka 2024, mkataba uliotolewa kwa kampuni ya Adani ulifutiliwa mbali kufuatia malalamiko kuhusu ukosefu wa uwazi katika mchakato wake.
Upanuzi wa JKIA unatarajiwa kuanza wakati wowote mwaka huu huku serikali ikisisitiza kuwa mchakato wote unafanyika kwa kufuata taratibu za kisheria na uwazi.









