Jaji Gatembu Kairu amechaguliwa kuwa rais mpya wa mahakama ya rufaa nchini baada ya kushinda katika uchaguzi uliofanywa na majaji wa mahakama hiyo Jumatatu tarehe 22 Juni 2026.
Jaji Kairu alipata kura 26 kati ya kura 41 zilizopigwa, akiwashinda wagombea wenzake ambao ni jaji Lydia Achode, jaji Patrick Kiage na jaji Agnes Murgor.
Uchaguzi wake unaashiria mabadiliko muhimu ya uongozi katika mahakama ya pili kwa hadhi nchini, na unamweka katika nafasi ya kuongoza mahakama ya rufaa wakati ambapo idara ya mahakama inaendelea kushughulikia masuala tata ya kikatiba, uchaguzi na kesi za maslahi ya umma.
Uchaguzi huo ulifanyika kwa mujibu wa taratibu za ndani za mahakama za kumchagua mkuu wa mahakama ya rufaa.
Rais wa mahakama ya rufaa ana jukumu la kutoa uongozi wa kiutawala na kimahakama kwa majaji wanaohudumu katika mahakama hiyo, na pia ana nafasi muhimu katika usimamizi wa rufaa kote nchini.
Ushindi wa jaji Kairu unafuatia kinyang’anyiro cha ushindani mkali kilichowashirikisha baadhi ya majaji wenye uzoefu mkubwa zaidi katika mahakama ya rufaa nchini.
Jaji Kairu anakuwa akijaza nafasi iliyoachwa wazi baada ya kukamilika kwa muhula mmoja wa miaka mitano wa kuhudumu wa jaji Daniel Musinga.









