Sifuna Aelekea Mahakamani Kupinga Kuondolewa Kwake Kwenye Wadhfa wa Katibu Mkuu wa ODM.

0

 

Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna amesema kuwa atawasilisha kesi mahakamani kupinga uamuzi wa Chama cha ODM wa kumwondoa katika wadhifa wa Katibu Mkuu wa chama hicho.

Wakizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari Jumanne, Juni 23, jijini Nairobi, Sifuna na washirika wake wametaja hatua ya Kamati Kuu ya Kitaifa ya ODM (NEC) kuwa kinyume cha katiba wakiapa kuipinga kupitia njia za kisheria.

Katika taarifa iliyosomwa na Mbunge wa Suba Kusini, Caroli Omondi, vuguvugu hilo limeshutumu uongozi wa chama hicho kwa kurudia makosa yaleyale yaliyosababisha kuondolewa kwa Sifuna kama katibu mkuu wa chama hicho kisha kubatilishwa na Mahakama ya Migogoro ya Vyama vya Siasa.

“Jana jioni, tulifahamishwa kuhusu uamuzi wa Kamati Kuu ya Kitaifa (NEC) ya ODM unaodai kwa mara ya pili kumwondoa Katibu Mkuu Edwin Sifuna ofisini. Kwa mtazamo wa kwanza, uamuzi huo ni sawa na ule uliofanywa Februari, ambao haukuwa wa haki na kinyume cha katiba,” Omondi alisema.

Aidha limesisitiza kwamba uamuzi wa hivi majuzi wa mahakama ulikuwa na dosari kisheria wakionyesha imani kwamba mahakama wakati huu itatoa uamuzi tena utakaompendelea Sifuna.

Pia limetangaza kuhairishwa kwa mikutano yake iliyopangwa ya Linda Mwananchi huko Kisii na Keroka kutoka Juni 26 hadi Julai 3.

Kulingana nao, uamuzi ulifanywa ili kuwaruhusu wanachama kujiunga na Wakenya kuadhimisha siku ya kumbukumbu ya maandamano ya Gen Z na kusimama kwa mshikamano na waathiriwa wa maandamano ya mwaka jana.

“Tunataka kuwafahamisha wanachama wetu, wafuasi wetu, na nchi kwa ujumla kwamba mikutano yetu ya Linda Mwananchi iliyopangwa kufanyika Juni 26 imehairishwa hadi Julai 3. Tutaungana na Wakenya katika kusimama pamoja na waathiriwa wa maandamano ya Gen Z,” taarifa hiyo ilisema.

Viongozi hao pia wameibua wasiwasi kuhusu kile walichokitaja kama ripoti za matumizi ya nguvu kupita kiasi yaliyopangwa dhidi ya waandamanaji, wakionya asasi za usalama dhidi ya kutumia nguvu kupita kiasi wakati wa maandamano hayo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here