Baraza la kitaifa la usalama limewatahadharisha viongozi dhidi ya kuchochea joto la kisiasa nchini miaka miwili kabla ya uchaguzi mkuu.
Akiwahutubia wanahabari baada ya mkutano wa baraza hilo, mkuu wa utumishi wa umma Joseph Kinyua amesema watakaopatikana na hatia ya kukiuka maagizo yaliyotolewa wataadhibiwa vikali pasipo kuzingatia hadhi yao katika jamii.
Miongoni mwa vigezo ambavyo viongozi wametakiwa kuzingatia ni pamoja na kuepuka uchochezi wakati wa mikutano yao, kukoma kuwatusi wenzao na kuheshimu maoni ya wenzao hata kama hawakubaliani nayo.
Wanaotumia mitandao ya kijamii vile vile hawajasazwa huku wakionywa dhidi ya kuchapisha taarifa za kizushi kwani watachukuliwa hatua.
Wakati uo huo
Tume ya uwiano na utangamano wa kitaifa (NCIC) imeelezea wasiwasi wake kuhusu uwezekano wa kutokea kwa machafuko ya kisiasa nchini iwapo wanasiasa hawatatuliza joto la kisiasa nchini.
NCIC kupitia mwenyekiti wake kasisi Samuel Kobia badala yake imetoa changamoto kwa viongozi kuwa katika mstari wa mbele kuwaunganisha Wakenya na wala sio kuwagawanya.
Tume hiyo aidha imewasihi vigogo wa kisiasa kuonyesha uongozi na kuwa kielelezo chema kwa wafuasi wao kwa kuepuka siasa za mgongano.









