Wanafunzi wang’ang’ania taasisi za chini licha ya kufuzu Digrii

0
Dr. Agnes Wahome, afisa mkuu mtendaji (KUCCPS) wakati wa matangazo ya nafasi za kujiunga vyuo.

Zaidi ya wanafunzi 293,000 waliofanya mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha nne (KCSE) mwaka 2025 wamepata nafasi za kujiunga na taasisi za elimu ya juu baada ya bodi ya uteuzi wa wanafunzi kujiunga na taasisi za juu za masomo (KUCCPS) kutangaza matokeo ya upangaji wa wanafunzi kwa mwaka wa masomo wa 2026/2027.

Matokeo hayo yalitangazwa na waziri wa Elimu, Julius Ogamba ambapo jumla ya wanafunzi 980,535 waliofanya mtihani huo walipewa fursa ya kutuma maombi ya kozi walizozichagua kupitia mfumo wa mtandaoni wa KUCCPS.

Kati yao, wanafunzi 270,508 waliopata alama ya C+ ya kujiunga na vyuo vikuu walipewa nafasi ya kutuma maombi ya programu za shahada huku waliosalia wakiomba kujiunga na kozi za elimu ya ufundi (TVET).

Kwa jumla, KUCCPS imewapa wanafunzi 293,869 nafasi katika programu za shahada, diploma za ngazi ya sita, vyeti vya ufundi vya ngazi ya tano na vyeti vya ufundi stadi vya ngazi ya nne katika vyuo vikuu na taasisi nyingine za elimu ya juu.

Kati ya waliopangiwa, wanafunzi 202,133 walipata nafasi katika programu za shahada, 28,246 Chuo cha Mafunzo ya utabibu (KMTC), 500 wamejiunga na programu ya stashahada ya sheria katika Shule ya Sheria (KSL), 765 wamepewa nafasi ya kujiunga na Kenya Utalii College, huku 875 wakipata nafasi katika vyuo vya mafunzo ya walimu wa shule za sekondari (TTC).

Waziri Ogamba amesema wanafunzi 8,915 waliokuwa wamehitimu kujiunga na programu za shahada walichagua kusomea kozi zisizo za shahada na wamepangiwa katika taasisi mbalimbali za elimu ya juu.

Ogamba alikiri kuwa si wanafunzi wote waliostahili waliotuma maombi ya kujiunga, akisema baadhi yao walichagua njia mbadala za kuendelea na elimu ya juu.

“Tunatambua kuwa baadhi ya wanafunzi waliostahili hawakutuma maombi kwa sababu walichagua njia nyingine za elimu na mafunzo. Baadhi wamejiunga na vikosi vya ulinzi na usalama, wengine wameenda kusoma nje ya nchi, huku wengine wakijiunga na programu za kujigharamia katika vyuo ambavyo havikupitia mfumo wa KUCCPS,” alisema Ogamba.

Aliongeza kuwa baadhi ya wanafunzi walishindwa kutuma maombi kutokana na sababu mbalimbali za kibinafsi.

“Nimeiagiza KUCCPS kuanzisha mpango wa kuwafuatilia wanafunzi hao. Na kwa wale waliokosa kutuma maombi kwa sababu nyingine yoyote, tutawapa nafasi nyingine ya kutuma maombi,” alisema.

Aidha alisema wanafunzi ambao hawajaridhishwa na taasisi au kozi walizopangiwa watapewa muda zaidi wa kuomba uhamisho.

“Dirisha la uhamisho kwa wanafunzi ambao hawajaridhishwa na taasisi walizopangiwa litaongezwa kutoka wiki mbili za kawaida hadi mwezi mmoja,” alisema.

Pia aliwahimiza wanafunzi wanaohitaji ufadhili wa serikali kutuma maombi yao bila kuchelewa.

“Mfumo wa ufadhili wa elimu ya juu sasa umefunguliwa kwa waombaji wapya kupitia tovuti za www.hef.co.ke au www.helb.co.ke. Wanafunzi wote wanaohitaji ufadhili wanashauriwa kutuma maombi haraka iwezekanavyo,” alisema.

Alibainisha kuwa Tume ya Elimu ya Vyuo Vikuu (CUE) iliidhinisha nafasi 327,157 katika vyuo vikuu 43 vya umma na 33 vya kibinafsi kwa mwaka wa masomo wa 2026/2027.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here