Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna ameondolewa rasmi katika wadhifa wa Katibu Mkuu wa Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) baada ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (ORPP) kuthibitisha uamuzi wa chama hicho na kusasisha rekodi zake rasmi za uongozi.
Hatua hiyo inahitimisha mvutano wa muda mrefu wa uongozi kati ya Sifuna na chama cha ODM, ambacho kupitia azimio la Kamati Kuu ya Kitaifa (NEC) kilikuwa tayari kimemwondoa katika nafasi hiyo.
Msajili wa Vyama vya Kisiasa John Cox Lorionokou katika barua iliyowasilishwa kwa Sifuna amesema kuwa, baada ya kupitia nyaraka zilizowasilishwa na chama pamoja na kutokuwapo kwa majibu kutoka kwa Sifuna, ilibainika kuwa kuondolewa kwake katika wadhifa wa Katibu Mkuu kulifanyika kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Kisiasa na Katiba ya ODM.
“Baada ya kupitia nyaraka zilizowasilishwa na chama pamoja na kutokuwapo kwa majibu kutoka kwa Sifuna, imsbainika kuwa kuondolewa kwake katika wadhifa wa Katibu Mkuu kulifanyika kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Kisiasa na Katiba ya ODM. Sura ya 7D, pamoja na Katiba ya Chama cha ODM,” amesema Msajili.
Aidha, amethibitisha kuwa mabadiliko hayo tayari yametekelezwa na rekodi rasmi za chama zimesasishwa kuonyesha uongozi mpya.
Hata hivyo, Sifuna amepinga uamuzi huo kupitia kwa wakili wake, Isaac Okero, ambaye ameishutumu Ofisi ya Msajili kwa kuchukua hatua hiyo kwa haraka bila kufuata kikamilifu taratibu zilizowekwa kisheria.
Katika barua yake kwa Msajili, Okero amesema kuwa hatua ya kusasisha rekodi za chama ilikiuka masharti ya Kifungu cha 20(2) cha Sheria ya Vyama vya Kisiasa, na hivyo kuifanya isiwe halali kisheria.
Ameongeza kuwa Sifuna ataelekea mahakamani kusaka suluhu.
Wakati huo huo, ODM imekaribisha uamuzi huo ikisema sasa chama kina nafasi ya kuendelea na shughuli zake baada ya mgogoro wa muda mrefu wa uongozi.
Akizungumza katika makao makuu ya ODM jijini Nairobi, Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho ambaye sasa ndiye Katibu mkuu na Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Busia, Catherine Omanyo, amesema chama kilisubiri kwa muda mrefu kupata idhini ya kuwaondoa viongozi ambao hawakuwa wakifuata msimamo wa chama.
“Hatungeweza kuendelea kuwa na mtu anayejitambulisha kama Katibu Mkuu ilhali anaendesha ajenda zake binafsi. Sasa chama kinaweza kuendelea na shughuli zake, naye yuko huru kuanzisha chama chake ikiwa anataka,” alisema Omanyo.
Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza mvutano wa kisiasa kati ya Sifuna na uongozi wa ODM huku seneta huyo akijiandaa kupinga uamuzi wa Msajili mahakamani.









