Ghasia Shuleni: Serikali Yaunda Kikosi Kazi cha Siku 90 Kusaka Suluhisho.

0

Waziri wa Elimu Julius Migos Ogamba ametangaza kuwa kikosi kazi maalum kilichoundwa kuchunguza ongezeko la visa vya ghasia shuleni kote nchini kitachapishwa katika Gazeti Rasmi la Serikali ndani ya wiki mbili zijazo.

Akizungumza katika Kaunti ya Nyeri Waziri Ogamba amesema kuwa kwa mara ya kwanza kikosi kazi hicho kitajumuisha wanafunzi na wazazi pamoja na wadau wengine wa sekta ya elimu.

Ameongeza kuwa kikosi kazi hicho kitafanya mashauriano ya umma kote nchini kabla ya kuwasilisha ripoti na mapendekezo yake ndani ya siku 90.

“Tunataka kuwa na kikosi kazi shirikishi kitakachowasikiliza wanafunzi, wazazi, walimu na wadau wote ili kubaini chanzo halisi cha ghasia shuleni na kutoa suluhisho la kudumu,” amesema Ogamba.

Waziri huyo pia ameonya kuwa watu watakaobainika kupanga, kufadhili au kuchochea visa vya ghasia shuleni watachukuliwa hatua kali za kisheria.

“Yeyote atakayebainika kupanga ghasia shuleni atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria. Hatutaruhusu uharibifu wa mali za shule wala kuvurugwa kwa masomo kuendelea,” amesema.

Ogamba pia amethibitisha kuwa uchunguzi kuhusu ghasia zilizotokea katika Shule ya Sekondari ya Nyabisase, Bobasi, umeimarishwa.

Tukio hilo lilianza kama maandamano ya kupinga kuhamishwa kwa Mwalimu mkuu wa shule, kabla ya kugeuka kuwa vurugu ambapo wanafunzi wanadaiwa kuwarushia walimu mawe na kuchoma bweni majira ya mchana.

Tukio hilo ni la hivi punde katika visa vya ghasia shuleni vinavyozua wasiwasi nchini, likijiri wiki chache baada ya mkasa wa moto katika Shule ya Utumishi Girls Academy, Gilgil, Kaunti ya Nakuru, uliosababisha vifo vya wanafunzi 16.

Kwa miaka mingi, Kenya imekumbwa na majanga ya Mikasa ya moto mashuleni, yakiwemo mkasa wa moto wa Shule ya Sekondari ya Kyanguli mwaka 2001 ulioua zaidi ya wanafunzi 60, mkasa wa moto wa Shule ya Msingi ya Wasichana ya Asumbi mwaka 2012 uliogharimu maisha ya wanafunzi wanane, wimbi la uchomaji wa shule zaidi ya 100 mwaka 2016, pamoja na mkasa wa moto wa bweni katika shule ya Hillside Endarasha Academy mwaka 2024 ulioua wavulana 21.

Wizara ya Elimu imehusisha ghasia hizo na sababu mbalimbali zikiwemo uongozi dhaifu wa shule, shinikizo la mitihani, mazingira duni ya mabweni, matumizi ya dawa za kulevya, ratiba ngumu za shule, ushawishi wa marafiki, tabia ya kuiga matukio ya wengine na madai ya baadhi ya wanafunzi kutaka shule zifungwe mapema.

Licha ya kuwepo kwa hatua mbalimbali za awali, zikiwemo Mwongozo wa Viwango vya Usalama Shuleni wa mwaka 2008, Kikosi Kazi cha Omolo cha mwaka 2016 na ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya mwaka 2020, wadau wa elimu wameendelea kusisitiza kuwa kinachohitajika ni utekelezaji wa mapendekezo yaliyopo badala ya kuunda vikosi kazi vipya ambavyo ripoti zake hazitekelezwi.

Serikali imesema kuwa matokeo ya kikosi kazi hicho yatasaidia kuongoza mageuzi ya muda mrefu yanayolenga kuimarisha usalama, nidhamu na mazingira bora ya kujifunzia katika shule zote nchini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here